Zingatieni sheria za kupiga kura – NEC

DAR-ES-SALAAM : TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imezitaka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
DAR-ES-SALAAM : TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imezitaka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Wito huo umetolewa leo Julai 30, 2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mkutano kati ya Tume na wadau hao wa elimu ya mpiga kura.
“Nitoe rai kwenu, hasa wale mliopewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura, kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo,” alisema Jaji Mwambegele.
Aliongeza kuwa Tume itashirikiana kwa karibu na taasisi na asasi hizo katika kipindi chote cha uchaguzi, huku akiwasisitiza kutowaacha nyuma wananchi katika kuwahimiza kutii sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi. SOMA: Uchaguzi Mkuu Oktoba 29
Aidha, alieleza kuwa kipindi cha kampeni huwa na joto la kisiasa kutokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu, hivyo taasisi hizo zina nafasi ya kuelimisha wananchi umuhimu wa amani na utulivu. “Kwenye majukwaa yenu, himizeni wananchi kuhakikisha kuwa hawawi chanzo cha vurugu. Ni muhimu uchaguzi ufanyike kwa amani,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa kifungu cha 10(1)(g)(h) na (i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, Tume ina wajibu wa kutoa na kuratibu elimu ya mpiga kura na kusimamia taasisi na asasi zinazotekeleza jukumu hilo.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Tume imetoa vibali kwa taasisi na asasi 164 kutoa elimu ya mpiga kura. Vilevile, taasisi na asasi 76 za ndani na 12 za kimataifa zimepewa kibali cha kuangalia uchaguzi.
Kwa upande wao, baadhi ya wawakilishi wa taasisi hizo wamesema wamejipanga kutoa elimu ya mpiga kura hasa kwa vijana wapiga kura wapya kwa mujibu wa sheria na maelekezo ya Tume.
Mwenyekiti wa Malezi Foundation Network, Mwalimu Neema Kabale, alisema taasisi yake imelenga kuwaelimisha vijana kuhusu mchakato wa kupiga kura ili washiriki kikamilifu kwa uelewa na uwajibikaji.