Wizara, PURA kuimarisha utoaji habari miradi ya mafuta, gesi

Habari Leo
Published: Oct 13, 2026 18:14:31 EAT   |  Educational

DAR ES SALAAM: Wizara ya Nishati na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) zimekutana kujadili mikakati ya kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia inayotekelezwa nchini. Majadiliano hayo yaliyofanyika Oktoba 13, 2026 katika Ofisi za PURA Jijini Dar es Salaam yalihudhuriwa na …

DAR ES SALAAM: Wizara ya Nishati na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) zimekutana kujadili mikakati ya kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia inayotekelezwa nchini.

Majadiliano hayo yaliyofanyika Oktoba 13, 2026 katika Ofisi za PURA Jijini Dar es Salaam yalihudhuriwa na wajumbe mbalimbali akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Nishati, Nteghenjwa Hosseah na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Charles Nyangi.

Akizungunza katika kikao hicho, Nteghenjwa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia lakini bado elimu kwa umma kuhusu miradi hii ni haijatolewa ipasavyi, hali inayofanya wananchi kutokuwa na uelewa mpana wa miradi inayotekelezwa.

“Kwa sasa tuna miradi inayoendelea kutekelezwa mkondo wa juu wa petroli ukiwemo mradi wa uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Lindi – Mtwara, mradi uchukuaji wa data za mitetemo za 2D katika Kitalu cha Eyasi – Wembere na maandalizi ya uchimbaji wa visima vya gesi asilia katika Kitalu cha Ruvuma. Hata hivyo, uelewa umma wa Watanzania kuhusu miradi hii na faida zake bado ni mdogo” alieleza Nteghenjwa.

Alisema pia pamoja na kwamba miradi hiyo inahusisha masuala ya kitaalamu, Wizara ya Nishati na Taasisi zake zinajukumu la kuhakikisha kuwa umma wa watanzania wanapata taarifa za utekelezaji wa miradi kwa lugha nyepesi na kwa wakati ili kusaidia kuongeza uelewa wao katika miradi hiyo.

Kwa upande wake, Nyangi amesema kuwa PURA itaendelea kuongeza nguvu katika utoaji wa habari kwa umma kuhusu miradi inayotekelezwa sambamba na kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu masuala ya mkondo wa juu wa petroli.

“Pamoja na kutumia vyombo mbalimbali vya habari katika utoaji wa taarifa, PURA imeendelea kuwezesha mafunzo kwa wanahabari na kutoa fursa kwa wanahabari kutembelea maeneo ambayo miradi ya mkondo wa juu wa petroli inatekelezwa nchini kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hawa muhimu katika kuhabarisha umma” aliongeza Nyangi.