Wawili wafa, 13 wajeruhiwa ajali ya basi Iringa
IRINGA: Watu wawili wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea asubuhi ya leo eneo la Mseke, wilayani Iringa, baada ya basi la kampuni ya Classic kugongana uso kwa uso na gari jingine kabla ya kupinduka na kutumbukia korongoni. Basi hilo, linalofanya safari kati ya Harare nchini Zimbabwe na Dar es …
The post Wawili wafa, 13 wajeruhiwa ajali ya basi Iringa first appeared on HabariLeo.
IRINGA: Watu wawili wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea asubuhi ya leo eneo la Mseke, wilayani Iringa, baada ya basi la kampuni ya Classic kugongana uso kwa uso na gari jingine kabla ya kupinduka na kutumbukia korongoni.
Basi hilo, linalofanya safari kati ya Harare nchini Zimbabwe na Dar es Salaam nchini Tanzania, lilipata ajali hiyo katika eneo hilo barabara kuu ya Iringa–Mbeya.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela, hospitali hiyo imepokea majeruhi 13, wakiwemo wanawake watatu na wanaume 10.
Alisema majeruhi watatu wako katika hali mahututi, akiwemo mwanamke mmoja mjamzito aliyepata jeraha kubwa la mgongo.
“Mmoja ameumia mbavu na damu kuvujia ndani ya kifua, huku wengine wakipata mivunjiko na majeraha mbalimbali. Wote wanaendelea kupatiwa matibabu chini ya uangalizi wa madaktari,” alisema Dk Mwakalebela.
Aidha, alisema baadhi ya majeruhi wanaweza kuruhusiwa kuanzia kesho kutwa endapo hali zao zitaendelea kuimarika.
Taarifa za hospitali zinaeleza kuwa mmoja wa waliofariki ametambulika kuwa ni Mtanzania anayeishi Tunduma, huku majeruhi wakijumuisha raia wanne wa Zambia na wanane wa Zimbabwe.
Ajali hiyo imetokea ikiwa ni wiki moja tangu ajali nyingine iliyohusisha basi la Shabiby na lori katika kijiji cha Tanangozi, kata ya Mseke, iliyosababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine 28.
Mamlaka zinaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo huku wananchi wakitakiwa kuendelea kuchukua tahadhari wanapotumia barabara.
The post Wawili wafa, 13 wajeruhiwa ajali ya basi Iringa first appeared on HabariLeo.