Waomba muziki uingizwe kwenye mtaala kukuza vipaji, ajira

Habari Leo
Published: Oct 08, 2026 08:25:48 EAT   |  Entertainment

DAR ES SALAAM; Wadau wa sekta ya muziki wameiomba  serikali kuingiza elimu ya muziki katika mtaala wa shule za msingi, wakisema hatua hiyo itasaidia kugundua na kukuza vipaji vya watoto mapema na kuwaandaa kutumia muziki kama taaluma na chanzo cha ajira. Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa kinanda kipya cha Yamaha PSR-SX620 Dar …

DAR ES SALAAM; Wadau wa sekta ya muziki wameiomba  serikali kuingiza elimu ya muziki katika mtaala wa shule za msingi, wakisema hatua hiyo itasaidia kugundua na kukuza vipaji vya watoto mapema na kuwaandaa kutumia muziki kama taaluma na chanzo cha ajira.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa kinanda kipya cha Yamaha PSR-SX620 Dar es Salaam, wadau hao walisema Tanzania ina vipaji vingi vya muziki vinavyohitaji kutambuliwa na kulelewa kupitia mfumo rasmi wa elimu.

Msimamizi wa Mauzo wa Yamaha Afrika, Moses Mbogo, alisema elimu hiyo itawasaidia watoto kutambua uwezo wao mapema na kupata ujuzi wa kuendeleza vipaji hivyo.

“Tunazungumzia fursa nyingi zilizopo kwenye sekta ya muziki. Tanzania ina muziki ambao unauza, hivyo vijana wakitumia vizuri fursa hizi wanaweza kufika mbali,” alisema.

Mbogo alisema muziki haupaswi kuangaliwa kama burudani pekee, bali taaluma inayoweza kutoa ajira na fursa za kujiajiri katika maeneo mbalimbali, ikiwamo uimbaji, utunzi, upigaji wa ala, utayarishaji na uhandisi wa sauti.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Topshop Music Limited, Aminmohamed Janmohamed, alisema Tanzania inahitaji kuongeza weledi katika sekta hiyo na kuwajengea watoto msingi wa muziki tangu wakiwa shuleni.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shifaa Pan African Hospitals Limited, Bashir Haroon, alisema utambuzi wa vipaji unapaswa kuanza utotoni badala ya kusubiri hadi vijana wafikie umri mkubwa.

“Mtoto akipewa nafasi mapema ya kujifunza muziki na kuonesha uwezo wake, tunaweza kugundua kipaji chake na kukilea vizuri,” alisema.

Alisema  kuingizwa kwa elimu ya muziki katika shule za msingi kunaweza kuwa sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya ubunifu na kuwaandaa vijana kutumia vipaji vyao kama rasilimali ya kiuchumi.