Wanyama waharibifu, wakali ‘wawekwa mtegoni’

Habari Leo
Published: Jun 06, 2025 08:38:37 EAT   |  Travel

TANZANIA imebarikiwa kuwa na maliasili nyingi wakiwamo wanyamapori ambao wamekuwa sehemu ya vivutio vya utalii nchini na kuliingizia taifa mabilioni ya fedha za kigeni kutokana na watalii wa ndani na nje ya nchi. Wanyamapori hao wamekuwa wakipatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi hususani katika hifadhi za taifa, lakini pia katika mapori ya akiba na maeneo …

TANZANIA imebarikiwa kuwa na maliasili nyingi wakiwamo wanyamapori ambao wamekuwa sehemu ya vivutio vya utalii nchini na kuliingizia taifa mabilioni ya fedha za kigeni kutokana na watalii wa ndani na nje ya nchi.

Wanyamapori hao wamekuwa wakipatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi hususani katika hifadhi za taifa, lakini pia katika mapori ya akiba na maeneo yaliyohifadhiwa ambako wamekuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

Idadi ya wanyamapori hao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na uhifadhi mzuri unaofanywa na wataalamu wa uhifadhi nchini, pamoja na hatua zilizochukuliwa na serikali kudhibiti ujangili nchini.

Hata hivyo, katika siku za karibuni kumekuwa na changamoto ya wanyamapori wakali ambao wamekuwa wakisababisha madhara kwa jamii zinazozunguka hifadhi. Wawakilishi wa wananchi (Wabunge) ni baadhi ya wadau ambao wamekuwa wakizungumzia vitendo hivi vya wanyamapori wakali na kuishauri serikali kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na wanyamapori hao wakali.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka wa fedha 2023/2024, Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate anaiomba serikali iwapatie tembo uzazi wa mpango ili kupunguza kasi ya kuzaliana. Mbunge huyo kutoka Mkoa wa Kagera anasema hakuna namna nyingine kama serikali inashindwa kuvuna tembo ambao wamekuwa hatari kwa maisha ya binadamu.

Serikali kwa upande wake inasema na imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuhakikisha wanyamapori hawa wakali hawaendelei kuwa tatizo kwa jamii zinazozunguka hifadhi.

Akiwa ziarani mkoani Tanga, Februari mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan anasema serikali inaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu huku akiielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia namna ya kupitia upya kanuni za malipo ya kifuta jasho.

Anaysema hayo Februari 24,2025 katika ziara alipokuwa akizungumza na wananchi wa Lushoto Mjini mkoani Tanga. “Tunaendelea kuongeza askari wanyamapori na kubuni mbinu mbalimbali za kufukuza wanyama wakali na waharibifu ikiwa ni pamoja na kutumia ndegenyuki (drones),” anasema Rais Samia.

Katika hotuba yake ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni Dodoma hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana anasema kutokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na wizara yake kupitia taasisi zake za uhifadhi, serikali ilifanikiwa kudhibiti matukio 4,012 ya wanyamapori wakali na waharibifu.

“Aidha, katika jitihada za kuokoa maisha ya wananchi na mali zao wakati wa kudhibiti matukio hayo, wanyamapori wakali na waharibifu 296 walivunwa wakiwemo mamba 63, viboko 63, tembo 34, nyati 15, fisi 71, simba 10 na chui mmoja,” anasema Dk Chana.

Aidha, anasema simba 10 walihamishwa kutoka eneo la Kijiji cha Mdori na kupelekwa katika mapori ya akiba ya Rungwa (simba 6) na Pande (simba 4). Kadhalika, nyani 90 waliondolewa Geita Mjini na kupelekwa katika Msitu wa Hifadhi wa Kigosi na chui watatu wakaondolewa katika Kijiji cha Nyichoka na kuhamishiwa Hifadhi ya Taifa Serengeti (1) na Bustani ya Wanyamapori Ruhila (2).

Anaeleza kuwa, wizara imelipa Sh 4,604,909,750 ikiwa ni kifuta jasho na machozi kwa wananchi 16,939 walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu kwa matukio yaliyotokea katika kipindi cha mwaka 2021 hadi kufikia Aprili 2025 katika halmashauri 78.

Aidha, anasema wizara inaendelea na malipo ya kifuta jasho na machozi kiasi cha Sh 1,082,049,500 kwa wananchi 5,542 wa halmashauri za wilaya 18. “Serikali itaendelea kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha uharibifu unaosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu unadhibitiwa kwa kiwango kikubwa.”

“Nitoe rai kwa wadau wote kuiunga mkono serikali katika jitihada hizi,” anasema waziri huyo wakati akiwasilisha hotuba yake ya bajeti bungeni. Katika kuhakikisha serikali inaendelea kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, Dk Chana anabainisha mikakati kwa mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026 kuhusu namna bora zaidi ya kuendelea kuwakabili wanyamapori hao wakali na waharibifu.

Anasema wizara kwa kushirikiana na wadau itawajengea uwezo askari wanyamapori wa vijiji 100 ili kukabili matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika halmashauri za wilaya 20.

“Vilevile, wizara itafanya semina pamoja na kununua pikipiki 22 kwa ajili ya maofisa wanyamapori wa wilaya 22 ili kuendelea kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu ao na kuwawezesha kufika katika maeneo ya matukio kwa wakati,” anasema Chana.

Kwa mujibu wa waziri huyo, katika kuimarisha ushiriki wa jamii katika uhifadhi, wizara itaendelea kuwezesha uanzishaji wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori nne katika wilaya za Uvinza, Mkalama, Kilolo na Ikungi. Aidha, wizara itaendelea kujenga uwezo kwa WMA mpya na zilizopo kwa kuziwezesha vitendea kazi zikiwemo pikipiki 12 ili kuimarisha ulinzi wa wanyamapori.

Vilevile, wizara itaendelea kuandaa miongozo mbalimbali ili kutatua changamoto za usimamizi wa WMA nchini. Dk Pindi anataja mikakati mingine kuwa ni pamoja na wizara kuendelea kutumia teknolojia katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa kununua ndegenyuki 12 na mikanda maalumu ya mawasiliano 50 kwa ajili ya ufuatiliaji wa mienendo ya wanyamapori hao.

“Mikanda hiyo itafungwa kwa tembo viongozi katika maeneo yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu,” anasema Dk Chana.

Anaongeza kuwa, wizara pia itanunua na kusambaza mabomu baridi 40,000 katika maeneo yenye changamoto ya tembo. Katika hatua nyingine, anasema wizara itaendelea kufanya tafiti za kimkakati ili kugundua mbinu mpya za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.

Anasema wizara itaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuongoa Shoroba za Wanyamapori wa Mwaka 2022 – 2026 kwa kuendelea kuelimisha jamii zilizopo kwenye maeneo ya shoroba za wanyamapori.

Alizitaja shoroba hizo kuwa ni za Ziwa Manyara, Kwakuchinja, Serengeti Complex – Yaeda Chini, Nyerere Selous – Niassa, Ruaha – Rungwa – Udzungwa, Ruaha – Rungwa – Katavi Complex, Kilombero – Milima ya Udzungwa, Nyerere Selous – Wami Mbiki, Serengeti Complex – Longido, na Udzungwa – Mikumi.

Anasema wizara itaendelelea kufanya tathmini ya hali halisi ya maeneo hayo, kubainisha mipaka na kuweka mabango. “Wizara pia itaendelea kulipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi watakaoathirika na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za mwaka 2011 na marejeo yake ya mwaka 2024,” anasema waziri huyo.

Kwa mujibu wa Chana, ili kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori, wizara kupitia taasisi zake za uhifadhi itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kupambana na Ujangili wa Mwaka 2023-2033; Mpango wa Usimamizi wa Tembo wa Mwaka 2023-2033 pamoja na Mpango wa Taifa wa Kuongoa Shoroba za Wanyamapori wa Mwaka 2022-2026.

“Utekelezaji wa mipango na mikakati hii utawezesha kudhibiti matukio ya ujangili na biashara haramu ya nyara nchini pamoja na kuimarisha uhifadhi,” anasema.

“Aidha, wizara itafanya mapitio ya Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Sura ya 283 na Kanuni zake ili kuimarisha uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori,” anasema Dk Chana ambaye wizara yake imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii, kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii na kuongezeka kwa maduhuli ya serikali.

Aidha, vyanzo mbalimbali vinabainisha kuwa Tanzania imeendelea kutambulika na kung’ara kimataifa, kuimarika kwa ulinzi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori na mafanikio ya 4R za Rais Samia katika kukuza biashara
ya utalii kwa kuiwezesha sekta binafsi.