Wananchi Msangamkuu wasogezewa huduma za afya

Habari Leo
Published: Aug 16, 2026 12:47:44 EAT   |  News

WANANCHI wa Kata ya Msangamkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea Kituo cha Afya cha Msangamkuu, kilichogharimu zaidi ya Sh milioni 25, wakisema kimewaondolea changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya. Wakizungumza wakati Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alipotembelea kituo hicho, wananchi wamesema awali walilazimika kwenda …

WANANCHI wa Kata ya Msangamkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea Kituo cha Afya cha Msangamkuu, kilichogharimu zaidi ya Sh milioni 25, wakisema kimewaondolea changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Wakizungumza wakati Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alipotembelea kituo hicho, wananchi wamesema awali walilazimika kwenda Mtwara mjini au maeneo jirani kupata huduma za afya.

Mwananchi Salumu Mfaume amesema ujenzi wa kituo hicho umewarahisishia kupata huduma za afya karibu na makazi yao.

“Kwa sasa tunaishukuru Serikali kwa kuturahisishia kupata huduma hii hapa nyumbani. Tumeondokana na changamoto ya kwenda Mtwara mjini kufuata huduma za afya. Huduma ni nzuri na tunapofika hapa tunahudumiwa,” amesema.

Mwananchi mwingine, Abdallah Yusufu, amesema kabla ya ujenzi wa kituo hicho walikuwa wakitegemea huduma katika Zahanati ya Namela, ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikitoa matibabu madogo.

Amesema uwepo wa kituo hicho umewawezesha kupata huduma za afya kwa uhakika zaidi na kwa ukaribu.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Alfan Juma, amesema kituo tayari kimeanza kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo za wagonjwa wa nje (OPD), afya ya mama na mtoto, maabara pamoja na huduma za kujifungua.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Mohamed Sinani, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa urahisi.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Serikali inaendelea kutekeleza kipaumbele cha kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma nchini.