Wahitimu 258 wavuna ujuzi, maarifa GGML

GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imetoa mafunzo kwa vitendo kwa jumla ya wahitimu 258 wa fani mbalimbali waliopata fursa mgodini hapo tangu mwaka 2017 hadi 2024. Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Duran Achery ameeleza hayo Juni 06, 2025 katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu wengine 47 wa fani tofauti kwa ajili ya kupata …
GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imetoa mafunzo kwa vitendo kwa jumla ya wahitimu 258 wa fani mbalimbali waliopata fursa mgodini hapo tangu mwaka 2017 hadi 2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Duran Achery ameeleza hayo Juni 06, 2025 katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu wengine 47 wa fani tofauti kwa ajili ya kupata mafunzo kwa vitendo kwa mwaka 2025/26.
Duran amebainisha miongoni mwa wahitimu waliopatiwa ujuzi na maarifa kutoka GGML, kati yao asilimia 47 ni wanawake huku asilimia 53 ni wanaume hali inayodhihirisha usawa wa kijinsia.
Amesema dhamira ya GGML kutekeleza mpango huo ni kuendeleza dhana ya uwezeshaji jamii na kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kufanya kazi kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Duran ameziomba taasisi za umma na binafsi kuendelea kushirikiana pamoja na GGML kuwezesha mpango wa kuwaongeza maarifa na ujuzi kwa vitendo wahitimu wa vyuo uzalishe wasomi wenye uwezo zaidi.
Katibu wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema mpango huo wa GGML umepunguza uhaba wa wahandisi na wataalamu wa fani mbalimbali kwenye sekta ya madini.
Mkuu wa raslimali watu mafunzo na ujuzi wa Chama cha Waajiri Tanzania, Albert Rukeisa ameipongeza GGML kwa kulipa kipaumbele suala la usawa wa kijinsia kwenye mpango wa mafunzo kwa vitendo.
Albert amekiri GGML ni mdau muhimu katika kuendeleza taaluma ya usalama mahala pa kazi, kwa kulingana na mkataba wa ajira na mazingira ili kuzalisha kizazi chenye tija.
Amesema vyama vya waajiri wote vimeingia makubaliano ya kuendeleza ujuzi na maarifa kazini, na tayari wameunda mabalaza ya ujuzi kwa kuanza na sekta ya madini ili kufikia adhima ya uwezeshaji vijana.
Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba amesema mpango wa uwezeshaji ujuzi na maarifa ni matokeo chanya ya sera rafiki zilizowekwa na serikali kwa wawekezaji kufanya kazi kwa manufaa ya jamii nzima.
“Uwepo wa uwekezaji huu mkubwa katika taifa letu unaruhusu teknolojia kuingia pamoja na kuhamisha ujuzi na maarifa kutoka mataifa makubwa na kurithishwa kwa watanzania”, amesema.
Mmoja ya wahitimu 47 walionufaika na mpango huo mwaka 2025, Grace John amekiri mpango wa GGML utaimarisha taaluma zao na kuwawezesha kuingia kwenye soko la ushindani katika fani ya uhandisi.