Waandishi wa habari wanolewa huduma PSSSF
DAR ES SALAAM: Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa umma na wanachama kuhusu huduma, haki na wajibu unaotolewa na Mfuko huo. Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Agosti 17, …
DAR ES SALAAM: Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa umma na wanachama kuhusu huduma, haki na wajibu unaotolewa na Mfuko huo.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Agosti 17, 2026, yalifunguliwa na Meneja wa PSSSF Kanda ya Kinondoni, Bw. Costa Mpagike, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mpagike alisema lengo kuu ni kujenga na kuimarisha uhusiano wa kudumu kati ya PSSSF na vyombo vya habari ili kuwezesha utoaji wa taarifa sahihi kwa umma kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii.
“Kama mjuavyo, mafunzo haya ya siku mbili yanalenga kujenga na kuimarisha uhusiano wa kudumu na vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari, kuongeza uelewa wa umma na wanachama kuhusu shughuli za PSSSF, haki na wajibu wao kupitia mada mbalimbali za mafunzo, uzalishaji wa makala za uchambuzi na kupunguza upotoshaji wa taarifa” alisema Mpagike.
Aliongeza kuwa mbali na kuwapatia maarifa kuhusu mifumo na huduma za PSSSF, Mfuko unatamani washiriki wa mafunzo hayo wawe mabalozi wa kueneza taarifa sahihi za hifadhi ya jamii katika vyumba vya habari na kwenye jamii kwa ujumla.
“Tutawajengea uwezo ili muwe na taarifa sahihi kuhusu PSSSF na huduma zake, jambo ambalo litawarahisishia kuandika habari kwa ukweli, weledi na usahihi zaidi,” alisisitiza.
Baadhi ya washiriki walieleza kufurahishwa na fursa hiyo ya mafunzo, wakisema elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha kazi zao za uandishi wa habari, hususan katika kuripoti masuala ya hifadhi ya jamii.
Mratibu wa mafunzo hayo, Nevile Meena, amesema elimu waliyoipata iwasaidie katika shughuli zao za uandishi wa habari.
“Kama hujui kitu huwezi kuandika kwa usahihi, kama unafahamu jambo utaandika kwa usahihi, nawashukuru PSSSF kwa kutujengea uelewa, mimi binafsi nimekuwa mwandihi wa habari wa siku nyingi lakini kuna vitu vingine nimevifahamu sasa kujifunza hakuna mwisho. Naamini tutayatendea haki haya mafunzo na tutafanya vizuri katika kazi zetu,” amesisitiza Meena.
Mwandishi wa habari kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Zena Chande, alisema mafunzo hayo yamemsaidia kuongeza uelewa kuhusu huduma na mafao yanayotolewa na PSSSF.
“Kimsingi nimeongeza uelewa kuhusu namna PSSSF inavyotekeleza majukumu yake. Mambo tuliyojifunza hapa yatanisaidia kufanya kazi yangu kwa ubora zaidi. Kabla ya mafunzo haya sikuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kiinua mgongo, pensheni na sifa za kufaidika na mafao hayo, lakini sasa nimeelewa kwa kiwango kikubwa,” alisema Chande.
“Ni mafunzo yenye tija kubwa sana kwetu sisi waandishi wa habari ambao tuna nafasi kubwa ya kuwasiliana na jamii wakiwemo wanachama wa PSSSF,” amesema Julieth Robert, mwandishi wa habari wa ITV.
Kwa upande wake, mwandishi wa habari mkongwe ambaye kwa sasa ni mnufaika wa pensheni kutoka PSSSF, Beda Msimbe, alitoa ushuhuda kuhusu umuhimu wa pensheni katika maisha ya mstaafu.
“Hii pensheni inanisaidia sana katika maisha yangu ya kila siku. Baada ya kustaafu, changamoto za maisha zipo, lakini mimi ninafurahia kuwa mwanachama wa PSSSF. Sasa ni mstaafu ninayepokea pensheni kila mwezi. Kila inapofika tarehe 22 napokea ujumbe mfupi wa simu unaonijulisha kuwa fedha zimeingizwa kwenye akaunti yangu. Kwa kweli, PSSSF wanatekeleza jukumu lao vizuri,” alisema Msimbe.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa PSSSF wa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, hususan vyombo vya habari, katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii na huduma zinazotolewa na mfuko huo.