‘Vipimo sahihi nguzo uchumi wa viwanda’

Habari Leo
Published: May 20, 2026 20:50:58 EAT   |  General

DODOMA :Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya vipimo nchini ili kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani katika soko la kimataifa, kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea sayansi na teknolojia. Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo wakati akifunga rasmi maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa …

The post ‘Vipimo sahihi nguzo uchumi wa viwanda’ first appeared on HabariLeo.

DODOMA :Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya vipimo nchini ili kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani katika soko la kimataifa, kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea sayansi na teknolojia.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo wakati akifunga rasmi maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa maendeleo ya viwanda, biashara na huduma bora hayawezi kufikiwa bila uwepo wa vipimo sahihi na vinavyoaminika.

Amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kisera na kisheria pamoja na vifaa vya kisasa kwenye taasisi za Vipimo ili kuwezesha biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza ufanisi wa sekta binafsi kwa kuzingatia matumizi ya vipimo vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

Hata hivyo amezitaka taasisi za serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana katika kuimarisha matumizi ya vipimo sahihi ili kuongeza uwazi, ufanisi na uaminifu katika maamuzi ya kitaifa.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Londo amesema Tanzania haiwezi kufikia uchumi wa viwanda na teknolojia bila kuwa na mifumo madhubuti ya vipimo, maabara za kisasa pamoja na wataalamu wenye ujuzi wa kimataifa kwani vipimo vina mchango mkubwa katika kuongeza tija viwandani, kuchochea ubunifu, kulinda afya za wananchi na kuimarisha biashara ya kimataifa.

Hata hivyo ameutaka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuendelea kusimamia haki katika matumizi ya vipimo ili wananchi wapate thamani halisi ya fedha wanazolipia na kudhibiti udanganyifu katika biashara.

Vilevile ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuendelea kuimarisha maabara za kitaifa, mifumo ya ithibati na ulinganifu wa vipimo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Kwa upande wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), amesema kinapaswa kuongeza programu za mafunzo zinazohusiana na vipimo, tathmini ya ubora na uandaaji wa sera ili kuzalisha wataalamu watakaosaidia kuunganisha sayansi na maendeleo ya uchumi.

The post ‘Vipimo sahihi nguzo uchumi wa viwanda’ first appeared on HabariLeo.