Vipaumbele 10 vya CHAUMMA kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

UBWABWA kwa wote, kilimo kwanza na nishati safi ndiyo baadhi ya ahadi zinazobeba ilani ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Katika kampeni zinazotarajiwa kuanza rasmi Agosti 28, mwaka huu chama hicho kimeweka mezani vipaumbele 10 vinavyoangazia uchumi jumuishi, ustawi wa wananchi, lishe bora, elimu bure yenye chakula …
UBWABWA kwa wote, kilimo kwanza na nishati safi ndiyo baadhi ya ahadi zinazobeba ilani ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Katika kampeni zinazotarajiwa kuanza rasmi Agosti 28, mwaka huu chama hicho kimeweka mezani vipaumbele 10 vinavyoangazia uchumi jumuishi, ustawi wa wananchi, lishe bora, elimu bure yenye chakula shuleni na matumizi ya teknolojia kuboresha maisha ya Watanzania.
Makala hii itaangazia kwa undani ahadi na vipaumbele vitakavyobeba ilani ya Chaumma kuelekea uchaguzi mkuu ambayo ndiyo kigezo cha kupima utekelezaji wa ahadi zao wakishapata madaraka.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, kipaumbele cha kwanza ni kukuza uchumi jumuishi kwa kufungamanisha sekta za uzalishaji na biashara kwa lengo la kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja. Ilani hiyo imetaka kipaumbele cha pili kwa serikali ya chama hicho kuwa ni kuboresha ustawi wa maisha ya Watanzania na kuondoa umasikini wa kipato kwa watu na mtu mmoja mmoja.
Jambo jingine ni kuwa na uongozi unaozingatia maadili, utii wa haki za binadamu na utawala wa sheria. Pia, Chaumma inasema katika miaka mitano ya utawala wake, itaweka sera na mifumo rafiki ya kodi, tozo na ushuru ili kupunguza ugumu wa maisha na kuvutia wawekezaji nchini.
Kipaumbele kingine ni kukifanya kilimo kuwa njia kuu ya kukabiliana na umasikini wa kipato na kuwezesha taifa kuwa na chakula cha kutosha, cha uhakika wakati wote. Katika kipaumbele cha sita, ilani ya Chaumma imejikita katika kutumia fursa ya teknolojia kujenga uchumi shirikishi na jumuishi na cha saba, ni kuhuisha na kukamilisha upatikanaji wa katiba na sheria za uchaguzi.
Chama hicho chenye wanachama zaidi ya 85,000 kimesema endapo kitashika madaraka katika siku 100 za kwanza kinaahidi kutekeleza mambo mbalimbali ya kisera na kisheria ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Ardhi kuchunguza mgogoro wa wananchi na mamlaka za uhifadhi za taifa za wanyamapori na mamlaka nyingine zinazohusika na masuala hayo ili kuondoa tatizo la mauaji ya wananchi wanaoishi au kupakana na hifadhi za wanyamapori au za misitu.
Inabainisha kuwa tume hiyo itachunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa muda mrefu imelitafuna taifa katika maeneo mbalimbali nchini bila kuwa na ufumbuzi wa kudumu.
Chaumma inaahidi kuanzisha na kuzindua mkakati wa mfumo bora wa lishe nchini ili kuhakikisha wananchi wote wanapata lishe bora kuanzia watoto wadogo katika ngazi ya elimu ya awali, wanafunzi shuleni na wagonjwa katika hospitali za umma.
Inaeleza kuwa mkakati huo utaitwa ‘Ubwabwa kwa wote’ ambao utaboresha mfumo wa lishe ili kuhakikisha taifa linaondokana na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe nchini.
Pia, inaahidi kuwasilisha Bungeni muswada wa kufuta tozo zote zinazoathiri sekta ya kilimo na ufugaji, tozo hizo zimeathiri mapato kwa wakulima na upatikanaji wa chakula bora na nyama nchini jambo litakalorudisha nyuma mkakati wa upatikanaji wa ubwabwa kwa wote.
Chama hicho kinaahidi kutunga sheria ya kuhuisha mfumo mzima wa serikali za mitaa, kimuundo na kimapato ambapo watalenga kufanya marekebisho ya utaratibu wa tozo na mapato ya halmashauri na Serikali kuu ili kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato na kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu.
Chaumma inasema endapo itashika madaraka itatunga sheria ya matumizi ya akili mnemba katika shule na vyuo bila kuathiri masuala ya ubunifu na uwezo wa kufikiri upya ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayokua kwa kasi duniani.
Inataja eneo mengine ni madini, ujenzi na makazi, maliasili na utalii, biashara, mazingira, kodi mbalimbali, ardhi na maendeleo ya watu.
Eneo jingine linalotajwa kwenye ilani hiyo ni kilimo ambalo Chaumma inaahidi kutenga asilimia 10 au zaidi ya bajeti yote ya nchi katika kilimo, ili kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika pato la taifa kwa kuweka miundombinu bora ya kilimo cha umwagiliaji.
Chaumma kinasema katika utekelezaji wa ilani hiyo itaweka msisitizo kwenye maeneo kumi ambayo ni utawala bora na haki za binadamu, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mfumo wa utawala, uchumi za Zanzibar, uchumi wa bahari na mafuta na gesi.
Maeneo mengine ni mgawo wa mapato yatokanayo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na mikopo na misaada kutoka nje. Pia, kitaweka msisitizo katika maeneo ya utamaduni na michezo Zanzibar, uchumi wa bahari, sekta ya afya na sekta ya biashara.
Katika sekta ya afya Chaumma inaahidi kuongeza bajeti za afya za kila mwaka ili kufikia Azimio la Abuja la kutenga asilimia 15 ya bajeti yote ya nchi katika afya na kuhakikisha kila Mtanzania anajumuishwa katika mpango wa bima ya afya.
Kwa wote na anapata huduma zote bora na za msingi za afya bila kujali kipato chake. Sambamba na hayo, ilani hiyo inaeleza kuwa itahakikisha huduma ya chakula kwa wagonjwa katika hospitali zote nchini inajumuishwa katika bima kama huduma ya lazima ya afya.
Kwenye sekta ya elimu inaahidi kuajiri walimu wa kutosha ili kuboresha uwiano mzuri wa mwalimu kwa wanafunzi wasiozidi 45 darasani. Pia, chama hicho kinaahidi kuwa na mfumo wa kutoa chakula bora katika shule zote za serikali za msingi na sekondari, kuboresha miundombinu ya maji safi na salama mashuleni pamoja na kuhakikisha vyoo vya shule zote ni safi na salama.
Aidha, kuhakikisha kunakuwa na ruzuku itakayogharamia upatikanaji wa taulo za kike ili kulinda utu, afya na heshima ya mtoto wa kike shuleni. Chama hicho kinasema katika sekta ya ardhi kitafuta kodi, tozo na ada zote zinazotozwa kwa ajili ya uandaaji wa hatimiliki na kuhakikisha hatimiliki zinatolewa bure kwa kila mwananchi baada ya eneo lake kupimwa.
Ilani hiyo inasema katika sekta ya lishe kwa wote itafuta kodi zote katika vyakula ili kuhakikisha vyakula vinapatikana kwa bei nafuu na kuanzisha sera na mkakati wa lishe kwa wote (ubwabwa kwa wote) ili kuhakikisha kila Mtanzania, hususani wanafunzi, wazee, wagonjwa na wajawazito wanapata lishe bora na kwa wakati.
Pia, kinaahidi kuanzisha huduma za matibabu mtandaoni katika maeneo ya vijijini na visiwani na wagonjwa wataunganishwa na madaktari bingwa kupitia simu au video ili kupunguza gharama na umbali wa kusafiri kufuata huduma.
Katika Sekta ya Nishati, Chaumma kinaahidi kupunguza gharama za kuunganishiwa umeme kwa wananchi, shule na zahanati kwa kuweka mfumo wa kulipia kidogo kidogo.
Ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kupikia, Chaumma kinasema kitaelekeza serikali kuondoa ushuru kwenye vifaa vya gesi, majiko banifu na vifaa vya nishati jadidifu.
Kinasema katika kuboresha sekta ya biashara kitahakikisha kinafanya mapitio na kuboresha upya ya sera na sheria rafiki za biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kutunga sera, kanuni na sheria zitakazobadilika mara kwa mara ili kujenga imani kwa wawekezaji.