Viongozi wa dini Kimara wapewa msaada wa vyakula
DAR ES SALAAM: Masheikh, walimu wa madrasa na viongozi wa dini katika Kata ya Kimara, Dar es Salaam, wamepatiwa tani moja na kilo 400 za mchele na kiasi kama hicho cha unga kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino. Msaada huo umetolewa na mfanyabiashara, mkulima na mchimbaji wa …
DAR ES SALAAM: Masheikh, walimu wa madrasa na viongozi wa dini katika Kata ya Kimara, Dar es Salaam, wamepatiwa tani moja na kilo 400 za mchele na kiasi kama hicho cha unga kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino.
Msaada huo umetolewa na mfanyabiashara, mkulima na mchimbaji wa madini, Dennis Mguye maarufu King Papa, wakati alipokutana na viongozi hao wa dini, akisema ameamua kuwafariji kutokana na mchango wao katika kuelimisha jamii bila kutegemea malipo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mguye amesema ametoa chakula hicho pia kutokana na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu mvua za El Niño, hivyo kuona umuhimu wa jamii kuwa na maandalizi ya chakula endapo kutatokea changamoto zinazoweza kuathiri maisha ya wananchi.
Amesema ni muhimu kwa watu wenye uwezo kujenga utamaduni wa kuwajali na kuwasaidia wengine katika maisha ya kila siku, akitoa wito kwa wafanyabiashara, wabunge, madiwani na viongozi wengine kutumia nafasi walizonazo kusaidia jamii badala ya kuwafikia wakati wa kampeni pekee.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA Kata ya Kimara, Khamis Rashid, amesema kitendo hicho ni mfano kwa watu wengine ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia uwezo wa kutoa kwa ajili ya jamii, huku akimshukuru mfanyabiashara huyo kwa kuwajali viongozi wa dini.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mavurunza, Batista Chang’a, amesema msaada huo si mara ya kwanza kutolewa na Mguye, akieleza kuwa amekuwa akisaidia jamii hiyo zaidi ya mara tatu au nne na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia moyo wa kusaidia watu.