Vijana watajwa nguzo ya soko la mitaji

Habari Leo
Published: Oct 13, 2026 10:30:16 EAT   |  Business

DAR ES SALAAM: SOKO la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limewataka vijana kuongeza ushiriki wao katika masoko ya mitaji, likisema kundi hilo lina nafasi muhimu katika kukuza uwekezaji na kuimarisha maendeleo ya soko la fedha nchini. DSE imesema kuongezeka kwa vijana wanaojihusisha na biashara ya hisa ni fursa ya kujenga utamaduni wa uwekezaji, kupanua …

DAR ES SALAAM: SOKO la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limewataka vijana kuongeza ushiriki wao katika masoko ya mitaji, likisema kundi hilo lina nafasi muhimu katika kukuza uwekezaji na kuimarisha maendeleo ya soko la fedha nchini.

DSE imesema kuongezeka kwa vijana wanaojihusisha na biashara ya hisa ni fursa ya kujenga utamaduni wa uwekezaji, kupanua ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji na kuandaa kizazi chenye uelewa wa masuala ya fedha kitakachochangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa kampeni ya Ring the Bell for Financial Literacy iliyofanyika Ijumaa, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa DSE, Emmanuel Nyalali, amesema vijana ni muhimu katika kuhakikisha soko la mitaji linaendelea kukua na kuwa endelevu.

Amesema takribani asilimia 40 ya washiriki katika shughuli za biashara ya hisa na dhamana nyingine katika soko hilo ni vijana wenye umri wa miaka 20 hadi 39, jambo linaloonesha kuongezeka kwa hamasa yao katika kutafuta fursa za uwekezaji.

“Hii inaonesha kuwa mustakabali wa soko hili ni endelevu kwa sababu vijana wanazidi kuonesha nia ya kushiriki katika soko,” amesema Nyalali.

Ameeleza kuwa ukuaji huo umechangiwa kwa sehemu na kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali wa Hisa Kiganjani, ambao umerahisisha upatikanaji wa huduma za soko la hisa kwa wawekezaji.

Nyalali amesema DSE inaendelea kutumia mwamko huo kuwafikia vijana wengi zaidi, kuwafahamisha fursa za uwekezaji na kuwahamasisha kujenga tabia bora za kusimamia fedha zao mapema katika maisha.

Ameongeza kuwa vijana ni kundi muhimu katika uchumi wa nchi kwa kuwa wanapomaliza masomo huingia kwenye ajira, kuanzisha biashara na hatimaye kuwa wawekezaji wakubwa katika masoko ya mitaji.

Kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masoko ya mitaji na umuhimu wa elimu ya uwekezaji. Juhudi hizo zinafanyika pia katika masoko mbalimbali ya hisa duniani kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuelewa fursa za uwekezaji na namna ya kuzitumia.

Kwa upande wake, William Idi, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mikocheni, amesema elimu ya fedha itawasaidia wanafunzi kujenga utamaduni wa kuweka akiba, kujitegemea na kujiandaa kutumia fursa za uwekezaji watakapokuwa wakubwa.

Amesema elimu hiyo itawapa hamasa ya kuweka akiba ya fedha wanazopewa na wazazi wao, kupanga malengo yao ya kifedha na kujifunza kuwa wavumilivu wanapokutana na changamoto katika biashara na uwekezaji.