Vijana mikoa 4 kunufaika na mradi Dumisha Amani
MTWARA: Vijana 240 katika wilaya za Mtwara, Lindi, Songea na Kigoma wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi kupitia mradi wa ‘Dumisha Amani’ unaofadhiliwa na mashirika ya kimataifa ya UNPDF, UNDP-Tanzania na kampuni ya CPP. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Chuo cha VETA Mtwara, Ofisa Mkuza Mitaala Mwandamizi wa Mamlaka ya Elimu …
MTWARA: Vijana 240 katika wilaya za Mtwara, Lindi, Songea na Kigoma wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi kupitia mradi wa ‘Dumisha Amani’ unaofadhiliwa na mashirika ya kimataifa ya UNPDF, UNDP-Tanzania na kampuni ya CPP.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Chuo cha VETA Mtwara, Ofisa Mkuza Mitaala Mwandamizi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Alphoncina Mshana amesema mafunzo kwa vijana hao yatatolewa kwenye vyuo vya VETA katika wilaya husika na yatafanyika kwa muda wa wiki mbili yakihusisha stadi za ufundi umeme, maabara, upishi na upambaji.
Amesema katika Wilaya ya Mtwara pekee, vijana 60 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo.
Ameongeza kuwa, sambamba na stadi za ufundi, vijana hao pia watafundishwa ujasiriamali na stadi za maisha, ili kuwajengea uwezo wa kutumia ujuzi wao kuanzisha biashara ndogo ndogo zinazohusiana na sekta za uchumi wa buluu.
Mshana amewashukuru wafadhili hao akieleza kuwa uhusiano mkubwa upo kati ya amani na ujengeaji wa stadi na maarifa kwa vijana, kwani vijana wakipata ujuzi na elimu itakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa, watakuwa na uwezo wa kujipatia kipato na hivyo kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.
“Tunatambua mchango wenu mkubwa kwa kufadhili mafunzo haya ambapo vijana wetu wa Kitanzania ndio taifa la sasa watapata ujuzi, elimu pamoja na maarifa,” amesema Mshana.
Kwa upande wake Meneja Mradi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania, Lin Chen amesema mafunzo hayo hayajalenga kuwapatia ujuzi pekee, bali pia kuwajengea ufahamu juu ya kudumisha amani na jinsi ya kuepuka migogoro katika jamii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka kampuni ya China Petroleum Pipeline (CPP), Bai Zhengdshuai, amesema vijana ndiyo chachu katika uvumbuzi, ukuaji uchumi na maendeleo endelevu, na kuonesha furaha yake katika kuwezesha vijana kupata ujuzi kwa vitendo zaidi.