Vicky Kamata atoswa Geita

GEITA : MWANAMUZIKI Mkongwe nchini aliyewahi kutamba na kibao cha 'Wanawake na Maendeleo', Vicky Kamata ameshika nafasi ya nne kati ya wagombea nane wa nafasi mbili za ubunge wa viti maalum mkoa wa Geita.
GEITA : MWANAMUZIKI Mkongwe nchini aliyewahi kutamba na kibao cha ‘Wanawake na Maendeleo’, Vicky Kamata ameshika nafasi ya nne kati ya wagombea nane wa nafasi mbili za ubunge wa viti maalum mkoa wa Geita.
Matokeo ya uchaguzi huo uliofanywa na wajumbe wa Kamati Kuu ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Geita yameonyesha kuwa Vicky Kamata alipata kura 186 kati ya kura za wajumbe 955 walioshiriki uchaguzi huo.
Vicky aliwahi kuhudumu kama mbunge wa viti maalum mkoa wa Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vipindi viwili katika bunge la 9 na 10 kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2020. SOMA: Wagombea 8 UWT kuchuana Kagera
Msimamizi wa Uchaguzi huo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita ametangaza matokeo hayo majira ya saa tatu usiku wa Julai 30, 2025 katika ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana Nyakumbu mjini Geita.
Mhita amesema idadi kamili ya wajumbe halali wa uchaguzi Mkuu wa UWT Mkoa wa Geita ni 1,022 kati yao wajumbe 67 waliomba udhuru na kutoweza kushiriki uchaguzi kwa sababu mbalimbali ikiwemo dharura binafsi.
Amesema kati ya kura 955 zilizopigwa, kura zilizoharibika ni nne huku kura halali zilikuwa 951 ambapo aliyeongoza katika kinyang’anyiro hicho ni Regina Mkenze aliyepata kura 831 za uchaguzi huo.
Aidha ametaja mgombea aliyeshika nafasi ya pili ni mbunge wa viti maalum anayetetea kiti chake, Josephine Chagula aliyepata kura 654 na nafasi ya tatu ikishikwa na Catherine Mbumbe aliyepata kura 188.
Amebainisha wagombea wengine ni Janeth Kasobi aliyepata kura mbili, Mwanaidi Shekue kura saba, Naomi Maalim alipata kura 14 na Getruda Manyesha alipata kura 17.