Ushiriki wa wazawa waimarika sekta ya gesi asilia
DODOMA:Jitihada za Serikali za kuwawezesha Watanzania kushiriki katika shughuli za kiuchumi zimeendelea kuzaa matunda katika sekta ya gesi asilia, huku viwanda vya kuchakata gesi asilia vya Madimba na Songosongo vikiendeshwa na wazawa kwa asilimia 100. Akizungumza katika Kongamano la Tano la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati (Local Content) Mwaka 2026 jijini …
DODOMA:Jitihada za Serikali za kuwawezesha Watanzania kushiriki katika shughuli za kiuchumi zimeendelea kuzaa matunda katika sekta ya gesi asilia, huku viwanda vya kuchakata gesi asilia vya Madimba na Songosongo vikiendeshwa na wazawa kwa asilimia 100.
Akizungumza katika Kongamano la Tano la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati (Local Content) Mwaka 2026 jijini Dodoma, Ofisa kutoka TPDC, Eugene Isaya amesema mafanikio hayo yanaonesha hatua zilizopigwa katika kuwawezesha wazawa kushiriki katika sekta ya mafuta na gesi.
“Jitihada za Serikali za kuwezesha ushiriki wa Watanzania zimezaa matunda katika sekta ya gesi asilia, kwani viwanda vya kuchakata gesi asilia vya Madimba na Songosongo vinaendeshwa na wazawa kwa asilimia 100,” amesema Eugene.
Ameongeza kuwa ajenda ya ushiriki wa Watanzania inalenga kuongeza thamani inayobaki nchini kupitia ajira, matumizi ya malighafi za ndani, ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani, ushiriki wa taasisi za Kitanzania pamoja na uhawilishaji wa teknolojia.
Katika kuunga mkono ajenda hiyo, TPDC imeshiriki na kudhamini kongamano hilo kwa kuchangia kiasi cha Shilingi Milioni Mia Moja (100).
Eugene ameongeza kuwa kuendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa kutasaidia kuongeza fursa kwa Watanzania katika sekta ya mafuta na gesi, kukuza uwezo wa wazawa na kuhakikisha manufaa yanayotokana na rasilimali zilizopo yanaendelea kuwafikia Watanzania.