Upanuzi Uwanja wa Ndege Musoma wafikia asilimia 70
MUSOMA: SERIKALI imefikia asilimia 70 ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Musoma mkoani Mara, unaogharimu Sh bilioni 36.3, huku ikielezwa kuwa ujenzi huo upo katika hatua za mwisho za kuukamilisha. Ufafanuzi huo umetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ambapo amesema serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa …
MUSOMA: SERIKALI imefikia asilimia 70 ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Musoma mkoani Mara, unaogharimu Sh bilioni 36.3, huku ikielezwa kuwa ujenzi huo upo katika hatua za mwisho za kuukamilisha.
Ufafanuzi huo umetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ambapo amesema serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Kihenzile amesema kukamilika kwa uwanja huo kutaboresha huduma za usafiri wa anga mkoani Mara na kuchochea shughuli za kiuchumi, utalii na biashara katika mkoa huo na maeneo jirani.
Amesema Serikali, kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), inalenga kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga katika Kiwanja cha Ndege Musoma kuanzia Septemba mwaka huu.
“Tunataka kuhakikisha wananchi wa Mara na maeneo jirani wanapata huduma bora na za uhakika za usafiri wa anga,” amesema.
Kwa mujibu wa Kihenzile, kuanza kwa huduma za ndege katika uwanja huo kutafungua fursa zaidi za kiuchumi na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, sambamba na kuimarisha shughuli za utalii na biashara.
Amesema baadhi ya miundombinu muhimu ya uwanja huo, ikiwemo njia ya kurukia na kutua ndege, maegesho ya ndege pamoja na maungio yake, imekamilika kwa asilimia 100.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga na kuongeza upatikanaji wa huduma za usafiri katika maeneo mbalimbali nchini.
Serikali imesema inalenga kuhakikisha Kiwanja cha Ndege Musoma kinaanza kutoa huduma kwa wananchi mara baada ya kukamilika kwa kazi zote zilizobaki.