Uhuru akejeli Ruto kuhusu dai kuwa yeye ni ‘sponyo’ wa Upinzani

Taifa Leo
Published: Sep 19, 2026 02:55:24 EAT   |  News

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta jana alimkejeli Rais William Ruto kuhusu madai yake ya mara kwa mara kwamba anafadhili upinzani, kwa kujitaja mwenyewe kama “Sponyo”. Bw Kenyatta alikuwa akizungumza katika mazishi ya Christine Waruguru, mama wa aliyekuwa Naibu Mdhibiti wa Ikulu George Kariuki, katika Kaunti ya Murang’a. Aliandamana na Naibu Kiongozi wa Jubilee Party na mgombea urais, Dkt Fred Matiang’i, pamoja na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro. Katika siku za hivi majuzi, Rais Ruto amekuwa akimtaja Bw Kenyatta kama mfadhili mkuu wa upinzani, wakati mwingine akimwita kiongozi wa waasi. Pia amekuwa akiita kundi la upinzani la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa “Linda Uhuru Kenyatta”. Katika hafla hiyo ya mazishi, Bw Kenyatta alianza kutoa hotuba bila maandishi kabla ya kujizuia na kusema imekuwa hatari kwake kutoa mawazo yake hadharani bila maandalizi. “Imekuwa hatari kwangu kuzungumza,nisije nikatafsiriwa vibaya na vyombo vya habari, acha nifuate rambi rambi zangu nilizoandika,” alisema. Baada ya kumaliza kusoma ujumbe wake wa rambirambi, alimalizia kwa kauli ya mzaha iliyowafanya waliohudhuria kuangua kicheko. “Hayo ndiyo machache kutoka kwa Sponyo,” alisema. Hafla hiyo pia ilikuwa muhimu kisiasa kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kwa Bw Kenyatta kushiriki jukwaa moja na Bw Nyoro tangu uhusiano wao wa kisiasa uvurugike mnamo 2018. Wakati huo, Bw Kenyatta alikuwa akimuunga mkono Raila Odinga kumrithi katika uchaguzi mkuu wa 2022, huku Bw Nyoro akiwa miongoni mwa viongozi wa Mlima Kenya waliomuunga mkono Dkt Ruto, ambaye wakati huo alikuwa Naibu Rais. Bw Nyoro alikuwa amechaguliwa kuwa Mbunge wa Kiharu mnamo 2017 kwa tiketi ya Jubilee akiwa mshirika wa karibu wa Bw Kenyatta. Lakini mnamo 2018, uhusiano wao ulianza kuvurugika. Wakati wa harusi ya aliyekuwa Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, ambaye sasa ni gavana, Bw Kenyatta aliwashauri viongozi chipukizi, akiwemo Bw Nyoro, kutulia na kuanzisha familia. Muda mfupi baadaye, uhusiano wa kisiasa kati yao ulizidi kuwa mbaya, huku Bw Nyoro akikamatwa kwa madai ya kutofautiana kisiasa na baadaye akamjibu Bw Kenyatta vikali katika kampeni. Uwepo wa Bw Nyoro jana uliongeza hamu ya kisiasa katika hafla hiyo, hasa kutokana na ukaribu wake wa hivi majuzi na Dkt Matiang’i. Bw Kenyatta alimuidhinisha Dkt Matiang’i kuwa chaguo lake la urais kuelekea uchaguzi wa 2027 katika hafla iliyofanyika Murang’a Novemba 7, 2025. Tangu wakati huo, Bw Nyoro amekuwa akionyesha kumuunga mkono Dkt Matiang’i, hali ambayo imeibua mjadala kuhusu uwezekano wa wawili hao kushirikiana katika uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, jana watatu hao hawakutoa tangazo lolote rasmi kuhusu mpango wa kisiasa au tiketi ya pamoja. Badala yake, Bw Kenyatta alizungumzia umuhimu wa taifa kuwaheshimu mashujaa wake, akisema Kenya ina historia ya kutowatambua ipasavyo waliotumikia taifa. Alisema wanawake na vijana ni miongoni mwa mashujaa ambao wamekuwa wakipuuzwa zaidi. Dkt Matiang’i naye alikosoa baadhi ya viongozi wa kitaifa ambao alisema wamekuwa wakiwatukana wengine, kuwadanganya wananchi na kutoa kauli zisizo na maana. Kwa upande wake, Bw Nyoro alimsifu Bw Kenyatta na kuhusisha baadhi ya miradi ya maendeleo katika Kiharu na uongozi wa rais huyo wa zamani. “Baadhi ya barabara mnazoona Kiharu zilitokana na uongozi wako mzuri, mkuu wangu,” alisema. Mbunge huyo pia alidokeza kuwa Bw Kenyatta bado ni mtu anayemshauri katika safari yake ya kisiasa. “Ninashukuru kwamba unatupa ushauri mzuri tunapokutafuta,” alisema. Bw Nyoro aliwaomba Wakenya kuelewa msimamo wake wa sasa wa kisiasa, akisema yuko katika hatua ya kujijenga mwenyewe.