TICD yaingiza moduli za PPP katika mitaala ya mafunzo
ARUSHA: Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) imefanya maboresho ya kimkakati katika mifumo yake ya mafunzo kwa kuingiza rasmi masuala na moduli za Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika mitaala ya programu zake za kitaaluma. Hatua hiyo inalenga kujenga jeshi la wataalamu wenye ujuzi wa kusimamia miradi ya kimkakati …
ARUSHA: Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) imefanya maboresho ya kimkakati katika mifumo yake ya mafunzo kwa kuingiza rasmi masuala na moduli za Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika mitaala ya programu zake za kitaaluma.
Hatua hiyo inalenga kujenga jeshi la wataalamu wenye ujuzi wa kusimamia miradi ya kimkakati nchini, huku ikiimarisha uwezo wa taasisi na wadau kushiriki kwa ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kaimu Naibu Mkuu (Mipango, Fedha na Utawala) wa TICD, Janeth Zemba, amebainisha hayo Ijumaa, Agosti 14, 2026, jijini Arusha katika mhadhara wa umma uliofanyika chuoni hapo.
Alisema uamuzi huo umechukuliwa ili kuhakikisha wahitimu wanaoingia katika soko la ajira wanakuwa na uwezo wa kuunganisha sekta ya umma, sekta binafsi na wananchi katika ngazi mbalimbali za maendeleo.
“Kutokana na maboresho hayo, programu za TICD sasa zinamwezesha mwanafunzi kuelewa mbinu za kuandaa maandiko ya miradi yenye tija na namna ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” alisema Zemba.
Alisema uwekezaji huo katika mafunzo unalenga pia kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha sekta binafsi kama injini ya ukuaji wa uchumi.
Alisisitiza kuwa ufundishaji wa moduli hizo unaendana na mwelekeo wa nchi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambapo miradi mingi ya kijamii na miundombinu inatarajiwa kutekelezwa kupitia ushirikiano wa kimkakati, badala ya kutegemea bajeti ya Serikali pekee.
“Tumechukua hatua hii ili kuunga mkono jitihada za serikali inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha matumizi ya ubia kama nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema.