‘The Royal Tour yapaisha mapato Selous’

Juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii kupitia filamu ya Tanzania; The Royal Tour, zimeongeza idadi ya Watalii katika Pori la akiba la Selous na kupandisha mapato kufikia bilioni 9.1 kwa mwaka wa fedha 2024/25. Ofisa Mhifadhi daraja la II na Ofisa Utalii Pori la Akiba Selous, Stephano Lukumay aliyabainisha hayo hivi karibuni …
Juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii kupitia filamu ya Tanzania; The Royal Tour, zimeongeza idadi ya Watalii katika Pori la akiba la Selous na kupandisha mapato kufikia bilioni 9.1 kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Ofisa Mhifadhi daraja la II na Ofisa Utalii Pori la Akiba Selous, Stephano Lukumay aliyabainisha hayo hivi karibuni alipozungumza katika kituo Cha Kingupira Wilayani Rufiji wakati wa kumuaga mmoja wa watalii waliotembele pori hilo, raia wa Marekani Hyk Aleksanyan.
Lukumay alimshukuru Rais Samia kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) ambayo ndiyo inasimamia pori hilo, kwa juhudi zake zilizochangia mafanikio hayo.
Akifafanua kuhusu mafanikio hayo Lukumai alisema kupitia filamu ya Royal Tour idadi ya watalii wanoatembelea pori hilo kwa utalii wa uwindaji imeongezeka kutoka watalii 104 mwaka 2021/22 hadi watalii 245 mwaka 2024/25.
Aidha anasema kwa ongezeko hilo mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 3.5 hadi Sh bilioni 9.1 katika kipindi hicho.
“Ni jambo la kipekee na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea wageni wengi zaidi katika Pori la Akiba Selous,” alisema Lukumay.
Kwa upande wake Aleksanyan ambaye alitembelea pori hilo kwa utalii wa uwindaji alinesha furaha yake kwa kufanikiwa kuua simba ambaye anasema hajawahi kumpata mahali kokote alikowahi kutembelea isipokuwa Selous.
“Nimekuja katika pori zuri la Selous Tanzania kwa ajili ya uwindaji halisi wa wanyamapori. Tanzania ni nzuri, nimekuwa katika nchi nyingi za Afrika lakini Tanzania inaonekana kuwa ndiyo iliyonivutia zaidi,” alisema.
“Kama nilivyosema kuna wanyamapori halisi, hakuna vijiji, ni eneo lenye wanyamapori tu. Nimekuwa na siku 21 hapa, ni siku nzuri zenye uzoefu wa kutosha, tumewinda sana, tumekuwa na siku ndefu za kutosha, tumekuwa tukitumia saa 16 kwa siku tukitafuta na kuwinda wanyama. Tulijitahidi kwa nguvu zote kutafuta Simba,” aliongeza.
Aliwahamasisha watu wengine kule Marekani waje na wafurahie kuona wanyamapori halisi na kuongeza kuwa Tanzania ni nchi nzuri na ya kustaajabisha hivyo watafurahi uwepo wao katika nchi hiyo.