TAWA waagizwa mbinu mpya za mapato ili kutoa gawio
ARUSHA: WAZIRI wa Maliasilia na Utalii, Dk Ashatu Kijaji ameiagiza Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) kuhakikisha inabuni vyanzo vipya vya mapato ili viakisi ukubwa wa jukumu la mamlaka hiyo ili ianze kutoa gawio kwa serikali. Dk Kijaji amesema hayo leo Januari 9, 2026 jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa bodi …
The post TAWA waagizwa mbinu mpya za mapato ili kutoa gawio first appeared on HabariLeo.
ARUSHA: WAZIRI wa Maliasilia na Utalii, Dk Ashatu Kijaji ameiagiza Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) kuhakikisha inabuni vyanzo vipya vya mapato ili viakisi ukubwa wa jukumu la mamlaka hiyo ili ianze kutoa gawio kwa serikali.
Dk Kijaji amesema hayo leo Januari 9, 2026 jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya TAWA na kusema kuwa katika mwaka 2024/25 idadi ya wageni waliotembelea maeneo yanayosimamiwa na TAWA kwa ajili ya utalii wa picha na uwindaji wa kitalii iliongezeka.
Amesema idadi iligikia watalii 240,967 ikilinganishwa na mwaka 2023/24 watalii 194,480 idadi ambayo haitoshi kulinganisha na jukumu la mamlaka hiyo.
Amesema juhudi za Serikali zilizolenga kuimarisha Sekta ya utalii ikiwemo kuondoa ukomo wa msimu wa uwindaji, kuongeza muda wa umiliki wa vitalu sambamba na kampeni maarufu ya Rais Samia Suluhu Hassan,“Tanzania the Royal Tour” na “Amazing Tanzania” shughuli za utalii katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA zimeendelea kuimarika.
Ameongeza bodi mpya inawajibu wa kuja na mpango kazi madhubuti wa kuongeza ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya ili mwaka huu waweze kutoa gawio kwa serikali.
Waziri Dk Kijaji amesema katika mwaka 2024/25, mapato yalifikia Sh bilioni 87.32 ikilinganishwa na Sh bilioni 75.96 zilizokusanywa mwaka 2023/24 kiasi hicho cha mapato bado hakikidhi mahitaji ya TAWA na serikali kwa ujumla.
Kijaji amesema Wizara na Serikali kwa ujumla ina matarajio makubwa na bodi hiyo katika kuongeza tija kwenye uhifadhi, idadi ya watalii, mapato na kutoa fursa zaidi kwa wananchi kunufaika na uwepo wa rasilimali ya wanyamapori katika maeneo yao.
Aidha, ameagiza katika kutekeleza majukumu wanapaswa kuzingatia kikamilifu maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kwa sekta ya Maliasili na Utalii kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/2030.
Ameitaka bodi kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia shabaha na malengo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Wizara itakuwa tayari muda wote kushirikiana na Bodi ya TAWA katika kutekeleza majukumu na kufanikiwa kwa TAWA ni mafanikio ya Serikali na wananchi kwa ujumla kwa kuwa katika kutekeleza malengo ya kiuhifadhi,” amesema Dk Kijaji.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula amesema bodi iliyoundwa imesheheni mchanganyiko wa watalaamu wabobezi wa Uhifadhi Misitu na Utalii wenye udhoefu wa Kitaifa na Kimataifa.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja General Mstaafu,Hamis Semfuko kwanza amemshukuru Rais kwa kumteua kwa awamu nyingine na kusema kuwa Bodi imejipanga kutekeleza mikakati ya miaka mitatu kuhakikisha mikakati yote ya Rais inatekelezwa.
“Tutafanya kazi kwa karibu na watumishi kuhakikisha uhifadhi unaimarika na mchango wa TAWA kwenye uchumi unaongezeka ili kufikia malengo ya ya serikali ya watalii milioni 8,” alisema Semfuko.
The post TAWA waagizwa mbinu mpya za mapato ili kutoa gawio first appeared on HabariLeo.