Tanzania yazidi kuvutia wawekezaji kimataifa

Habari Leo
Published: Sep 16, 2026 09:36:16 EAT   |  News

DAR ES SALAAM: TANZANIA imekuwa miongoni mwa nchi zinazovutia wawekezaji, baada ya kufanikiwa kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.7 ndani ya kipindi cha miaka mitano. Taarifa hiyo imetolewa leo, Septemba 16, 2026, na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya, katika uzinduzi wa Jukwaa la …

DAR ES SALAAM: TANZANIA imekuwa miongoni mwa nchi zinazovutia wawekezaji, baada ya kufanikiwa kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.7 ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Taarifa hiyo imetolewa leo, Septemba 16, 2026, na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya, katika uzinduzi wa Jukwaa la Uwekezaji lililoandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) jijini Dar es Salaam, linalojadili mifumo ya kisera, kimuundo na kiusimamizi katika uwekezaji, huku likiwakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 60 za Afrika, Amerika Kusini na Asia.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Dk. Chaya amesema TISEZA inaendelea kupokea wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini kutokana na Tanzania kuwa nchi salama, yenye sera zinazotabirika na mazingira yanayowezesha uwekezaji, huku akisisitia kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Serikali inalenga kufanya mabadiliko makubwa katika miundo, sheria na usimamizi wa uwekezaji ili kuongeza kiwango cha uwekezaji nchini.

Kwa mujibu wa Dk Chaya, baadhi ya hatua za maboresho hayo tayari zimeanza kutekelezwa, huku lengo likiwa ni kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza barani Afrika katika kuvutia uwekezaji.

“Tunataka uwekezaji uwe na tija kwa ajili ya kupunguza tatizo la ajira. Tuna vijana wengi ambao hawana ajira, hivyo kupitia uwekezaji tunaenda kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira nchini. Lakini kubwa zaidi, tunaenda kuimarisha mahusiano mazuri na nchi nyingine,” amesema Dk Chaya.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais anayesimamia Mikakati ya Kimataifa na Mkurugenzi Mtendaji wa IISD barani Ulaya, Nathalie Bernasconi, amesema nchi za Afrika zimeanza kutengeneza mifumo ya uwekezaji inayozingatia mazingira na mahitaji ya bara hilo.

Amesema baada ya nchi za Afrika kuandaa mifumo ya kikanda ya uwekezaji na baadaye mfumo wa uwekezaji wa bara kupitia Itifaki ya Uwekezaji ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), hazikuishia katika kuiga kanuni zilizotengenezwa katika maeneo mengine, bali zimeanza kuunda mifumo mipya inayozingatia mazingira yao.

Bernasconi amesema changamoto kubwa iliyopo ni kuhakikisha kanuni mpya za uwekezaji zinaendana na mifumo ya zamani iliyopo, ikiwemo mikataba ya uwekezaji na mifumo ya kutatua migogoro kati ya wawekezaji na Serikali.

Naye Mkurugenzi wa Uwekezaji Endelevu katika Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD), Suzy Nikièma, amesema lengo la jukwaa hilo ni kuwakutanisha watunga sera na wadau wa uwekezaji kutoka Afrika, Amerika Kusini na Asia ili kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika maeneo yao.

Amesema washiriki wanajadili pia vipaumbele vyao katika uwekezaji na namna ya kushirikiana ili kuhakikisha Serikali zinavutia uwekezaji wenye ubora na unaozalisha manufaa ya muda mrefu.

Kwa mujibu wa Nikièma, suala la uwekezaji halipaswi kuangaliwa kwa kuzingatia wingi wa mitaji unaoingia nchini pekee, bali pia namna uwekezaji huo unavyoongeza thamani katika uchumi wa ndani, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Hamis Shibu, amesema kongamano hilo litatoa fursa kwa Tanzania Bara na Zanzibar kujifunza na kufanya maboresho katika sheria na sera za uwekezaji kwa lengo la kuendelea kuvutia mitaji. Pia amesema bado kuna fursa kubwa ya kukuza uwekezaji nchini kupitia majukwaa na makongamano ya kimataifa yanayowakutanisha Serikali, wawekezaji na wadau wa sekta mbalimbali.

Amesisitiza kuwa mijadala ya aina hiyo ni muhimu katika kubaini changamoto zinazokabili mazingira ya uwekezaji na kutafuta suluhisho zitakazowezesha Tanzania kuendelea kuvutia uwekezaji wenye tija kwa uchumi na wananchi.