Tanzania yang’ara utalii duniani

TANZANIA imefanikiwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kuongeza mapato kupitia sekta ya utalii kwa asilimia 66 ikifuatiwa na Tunisia na Morocco. Imefanikiwa pia kuongeza idadi ya watalii kwa asilimia 50 na kuingia katika orodha ya nchi 20 bora duniani kuwa na ongezeko kubwa la watalii tangu 2019. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja …
TANZANIA imefanikiwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kuongeza mapato kupitia sekta ya utalii kwa asilimia 66 ikifuatiwa na Tunisia na Morocco.
Imefanikiwa pia kuongeza idadi ya watalii kwa asilimia 50 na kuingia katika orodha ya nchi 20 bora duniani kuwa na ongezeko kubwa la watalii tangu 2019.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism Q1, 2025) mpaka Mei 2025, Tanzania imeendelea kufanya vizuri kiutalii Afrika na duniani katika takwimu za robo ya kwanza ya 2025.
Ripoti hiyo imeonesha kuna ongezeko la watalii na mapato nchini ikilinganishwa na 2019 kabla ya janga la Uviko-19.
Ripoti hiyo pia ilionesha kuwa Tanzania imeingia katika tatu bora ya nchi za Afrika zinazoongoza kwa ongezeko la watalii wengi ikilinganishwa na 2019 kwa kupata ongezeko la watalii kwa asilimia 50 baada ya Morocco yenye asilimia 60 na Ethiopia yenye asilimia 52.
Takwimu hizo pia zinaonesha Tanzania ni nchi ya 12 duniani ikiwa katika orodha moja na mataifa kama Norway, Brazil, Qatar, Saudia, Moldova kama mataifa yaliyojiingizia mapato zaidi kupitia utalii.
Akizungumzia mafanikio hayo Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas alisema mafanikio hayo yanatokana na mikakati bora ya kuitangaza Tanzania kimataifa.
“Rais Samia Suluhu Hassan ametoka ofisini akaenda ‘field’ akafanya filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania viongozi wetu wa wizara, mabalozi wetu kote duniani, taasisi zetu na wadau wametoka kwenda kuitangaza nchi,” alisema.
Aliongeza: “Kwetu sisi maono ya kwenda mbele ni kuwaza mikakati zaidi ikiwemo kupitia kujitangaza kwenye ligi kubwa duniani. Ukiangalia ile ripoti utaona Qatar na Saudia wako juu ni matokeo ya mikakati pia ya vitu kama michezo na matamasha yanayofuatiliwa na nchi nyingi”.
Kadhalika Dk Abbas alisema kwa sasa Tanzania imefurika watalii waliokuja kutazama vivutio na kuchangia mapato.
Alisema kupitia taarifa iliyotolewa na Benki Kuu hivi karibuni sekta ya utalii imeingiza dola za Marekani bilioni 3.92 kwenye uchumi ikiwa namba moja kuleta fedha za kigeni huku makusanyo ya maduhuli kwa taasisi zote kubwa za utalii yamefikia viwango vya juu zaidi.
Dk Abbas alisema kupitia masoko makubwa nchi imejitangaza vya kutosha.
“Nchi ya Marekani ongezeko la watalii kuja Tanzania ni asilimia 41, China na India leo watalii kutoka China wameongezeka kwa asilimia 108 na kutoka India ni asilimia 75. Kona zote tunaona watalii na mapato vikiongezeka,” alisema.