Tanzania, Korea kushirikiana teknolojia ya madini
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni utekelezaji wa Madini Vision 2030, imewezesha kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha kisasa cha Teknolojia ya Madini pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa madini.
The post Tanzania, Korea kushirikiana teknolojia ya madini first appeared on HabariLeo.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni utekelezaji wa Madini Vision 2030, imewezesha kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha kisasa cha Teknolojia ya Madini pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa madini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe maalum wa wataalamu sita kutoka Korea Kusini, ulioongozwa na Seong-Jun Cho wa Taasisi ya Jiosayansi na Rasilimali Madini ya Korea (KIGAM).
Waziri Mavunde amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara ya Madini kuhakikisha eneo la utafiti wa madini linaongezeka hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, akibainisha kuwa mradi huo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali kufikia malengo hayo.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatokana na makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya KIGAM ya Korea Kusini kupitia Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa mwaka 2024.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mradi huo unatarajiwa kugharimu woni bilioni 21.8 za Korea, sawa na dola za Marekani milioni 16.5, na utahusisha ujenzi wa Kituo cha Teknolojia ya Madini, uchunguzi wa pamoja wa mfumo wa kidijitali wa taarifa za rasilimali madini, ujenzi wa uwezo kwa wataalamu pamoja na utekelezaji wa mifumo ya ESG katika sekta ya madini.
Ameongeza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kupanua matumizi ya teknolojia hiyo katika utafiti wa madini mengine ya metali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wachimbaji na wawekezaji. SOMA: Mavunde aonya maofisa madini wa mikoa
Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa Serikali inatekeleza mpango wa kuwawezesha vijana na wanawake katika sekta ya madini (MBT), na kuiomba KIGAM kusaidia zaidi katika ujenzi wa uwezo ili kufanikisha mpango huo. “Mradi huu pia utatoa fursa kwa wachimbaji wadogo kupata mafunzo yatakayoongeza ufanisi na tija katika shughuli zao,” alisema.
Awali, akitoa wasilisho kuhusu mradi huo, Msimamizi Mkuu wa KIGAM, Seong-Jun Cho, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na kueleza kuwa mradi huo, unaojikita zaidi kwenye madini ya nikeli, utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2027 hadi 2031 na kunufaisha Taifa.
The post Tanzania, Korea kushirikiana teknolojia ya madini first appeared on HabariLeo.