Takukuru yatumia ngoma za asili vita dhidi ya rushwa

Habari Leo
Published: Oct 19, 2026 17:17:40 EAT   |  News

IKUNGI, SINGIDA: Taasisi ya Kuzuia ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Singida imekuja na mbinu mpya ya kutumia ngoma za asili kuelimisha wananchi madhara ya rushwa na umuhimu wa uadilifu katika jamii. Hayo yamedhihirika wakati wa tamasha la la ngoma za asili lililofanyika katika kata ya Iyumbu, wilayani Ikungi, Singida mwishoni mwa juma ambapo vikundi …

IKUNGI, SINGIDA: Taasisi ya Kuzuia ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Singida imekuja na mbinu mpya ya kutumia ngoma za asili kuelimisha wananchi madhara ya rushwa na umuhimu wa uadilifu katika jamii.

Hayo yamedhihirika wakati wa tamasha la la ngoma za asili lililofanyika katika kata ya Iyumbu, wilayani Ikungi, Singida mwishoni mwa juma ambapo vikundi mbalimbali vilifanya maonesho kwa umahiri huku vikiweka msisistizo kwenye kauli mbiu ‘Ngoma Zetu, Uadilifu Wetu’.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha hilo, Mkuu wa Takukuru mkoani Singida, Sosthenes Kibwengo alisema kuwa jamii za Kitanzania zina utajiri mkubwa wa mila, desturi, nyimbo, ngoma na sanaa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika kuelimisha, kuonya, kukemea maovu na kuimarisha mshikamano.

“Kwa muda mrefu, ngoma za asili zimekuwa sehemu muhimu katika maisha yetu, zikitumika kufikisha ujumbe na kurithisha maarifa na maadili kutoka kizazi kimoja kwenda kingine,” Kibwengo alisema.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo, Takukuru imeamua kutumia ujumbe huo kuhamasisha matendo ya uadilifu kupitia utamaduni ili kujenga jamii inayojali haki, usawa na maendeleo.

“Napenda kutumia nafasi hii kueleza kuwa, uadilifu hauishi katika ofisi za Serikali pekee. Uadilifu unaanzia nyumbani, shuleni, katika bishara, kwenye shughuli za kijamii na katika maeneo yetu ya kazi,” alisisitiza mbele ya Katibu Tawala wa Halsmahauri ya Wilaya ya Ikungi, Rashidi Rashidi.

Aliongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanaanza na maamuzi wananchi wanayofanya kila siku hivyo wanapoikataa ina maana wanalinda haki zao na wakitoa taarifa za vitendo vya rushwa wanasaidia uwajibikaji.

“Natoa wito kwa wananchi wa Kata ya Iyumbu na Wilaya ya Ikungi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na TAKUKURU na viongozi wengine katika kujenga jamii inayokataa rushwa na kuthamini uadilifu,” aliongeza.

Alifafanua kuwa tamasha hilo ni zaidi ya burudani kwani jukwaa la kuunganisha utajiri wa utamaduni wetu na mapambano dhidi ya rushwa, kwa kutumia sanaa kama nyenzo ya kuelimisha jamii kuhusu madhara ya rushwa, kuhamasisha uwajibikaji na kujenga misingi imara ya uadilifu.

Alisema kuwa rushwa kikwazo cha maendeleo na hudhoofisha utoaji wa huduma bora, husababisha matumizi mabaya ya rasilimali za umma, hudhoofisha Imani ya wananchi kwa taasisi zao na inaweza kuwanyima wananchi haki wanazostahili.

Alifafanua kuwa madhara yake hugusa maisha ya kila siku ya wananchi, kuanzia katika huduma za afya na elimu hadi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.