Soko la Machinga matumaini mapya Iringa

Habari Leo
Published: Sep 17, 2026 07:02:13 EAT   |  Business

IRINGA: Matumaini ya wafanyabiashara wadogo mjini Iringa kupata eneo rasmi la kufanyia biashara yameongezeka baada ya kuwekwa wazi mpango wa ujenzi wa soko la Machinga la kisasa lenye thamani ya Sh bilioni 4.6. Soko hilo linatarajiwa kujengwa katika eneo ilipokuwa Stendi Kuu ya Mabasi ya mjini Iringa, likiwa miongoni mwa miradi inayolenga kuboresha mazingira ya …

IRINGA: Matumaini ya wafanyabiashara wadogo mjini Iringa kupata eneo rasmi la kufanyia biashara yameongezeka baada ya kuwekwa wazi mpango wa ujenzi wa soko la Machinga la kisasa lenye thamani ya Sh bilioni 4.6.

Soko hilo linatarajiwa kujengwa katika eneo ilipokuwa Stendi Kuu ya Mabasi ya mjini Iringa, likiwa miongoni mwa miradi inayolenga kuboresha mazingira ya biashara na kutoa fursa kwa machinga ambao kwa muda wamekuwa wakihangaika kupata maeneo rasmi ya kufanyia shughuli zao.

Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, alisema hayo wakati wa ziara yake ya kata kwa kata katika kata ya Mkwawa na Igumbilo, iliyolenga kusikiliza kero za wananchi na kuzifikisha katika mamlaka zinazohusika.

Alisema soko hilo litakuwa la kisasa, akifananisha na masoko yaliyojengwa katika Jiji la Dodoma na Dar es Salaam.

Mbunge huyo pia alisema anataka soko Kuu la mjini Iringa liboreshwe kwa kuvunjwa na kujengwa upya ili liendane na mahitaji ya sasa ya wafanyabiashara na wananchi.

Hatua hiyo, alisema, ni sehemu ya mtazamo wa kuboresha miundombinu ya biashara katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Akizungumzia ziara yake ya kata kwa kata, Ngajilo alisema wananchi wana nafasi kubwa katika kumsaidia kutekeleza wajibu wake wa uwakilishi kwa kutoa kero na mapendekezo yao.

“Nitumieni vizuri niwawakilishe vizuri. Maswali yenu yananipa njia ya kuwasumbua watendaji wa serikali. Kila nachosema lazima kitoke kwenu,” alisema na kuongeza kwamba kazi yake ni kusimamia maslahi ya wananchi na kufuatilia hoja wanazowasilisha.

Ngajilo alisema Jimbo la Iringa Mjini linaendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo, akitaja uwanja wa ndege wa Iringa na barabara ya mchepuo ya Igumbilo kuwa miongoni mwa miradi hiyo.

Alisema Sh bilioni 6 zimetolewa kwa ajili ya barabara hiyo na tayari inapitika, lakini bado kuna mahitaji makubwa ya fedha ili kukamilisha mradi huo. Jumla ya Sh bilioni 43 zitatumika kwa ujumla kukamilisha mradi huo.