Silaha fiche ya Sifuna akisaka chombo mbadala cha kuwania urais 2027
SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna na viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi wameanza kutekeleza mkakati wa pande mbili huku wakijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Huku kundi hilo likiendelea na mapambano ya kisheria kulinda jina la Linda Mwananchi, pia limeanzisha juhudi za kutafuta chama mbadala cha kisiasa litakalotumia ikiwa halitafaulu mahakamani.
Hatua hiyo inajiri huku muda wa kutimiza masharti ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ukiendelea kuyoyoma, jambo linaloweka presha kwa viongozi wa vuguvugu hilo kuhakikisha wana chama cha kisiasa cha kutumia kushiriki uchaguzi wa Agosti 10, 2027.
Jana, Jopo la Mahakama la kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) liliwapa afueni washirika wa Bw Sifuna baada ya kumzuia Msajili wa Vyama vya Kisiasa kusajili chama kipya kinachotumia jina la Linda Mwananchi au jina lingine linalofanana nalo hadi rufaa iliyowasilishwa na viongozi wa vuguvugu hilo isikizwe na kuamuliwa.
Uamuzi huo pia umeathiri mchakato unaoendelea wa kusajili chama cha Liberty National Democratic Alliance (LINDA) pamoja na jina la Mwananchi Party, huku ukiwalinda walalamishi dhidi ya uwezekano wa jina la Linda Mwananchi kutumiwa na kundi lingine.
Kesi hiyo imewasilishwa na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi, aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) Faith Odhiambo na mwanamikakati wa kisiasa Pauline Njoki Njoroge.
Watatu hao wanapinga jinsi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa ilivyoshughulikia ombi lao la kuhifadhi jina la Linda Mwananchi Movement.
Hata hivyo, huku kesi hiyo ikiendelea mahakamani, duru za karibu na vuguvugu hilo zinasema viongozi wake hawataki kutegemea matokeo ya mahakama pekee.
Tayari wameanza mazungumzo na baadhi ya vyama vya kisiasa vilivyosajiliwa kikamilifu kwa lengo la kuvibadilisha jina, rangi na uongozi ili viwe jukwaa lao la kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu.
Miongoni mwa vyama vinavyotajwa ni United Democratic Party (UDP), chama kilichohusishwa na mwanasiasa marehemu Cyrus Jirongo.
Chama hicho kwa sasa kinapitia mchakato wa kubadilishwa jina na kuwa Ukombozi People’s Party (UPP).
Kulingana na notisi ya umma iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Bernard Wafukho, kuna mipango ya kubadilisha rangi za chama, kaulimbiu na nembo yake.
Pia, chama cha United Patriotic Movement (UPM) kinachohusishwa na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale kimetajwa.
Kulingana na rekodi za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, UPM kilipata usajili kamili mnamo Juni mwaka huu.
Awali, Dkt Khalwale alidokeza kuwa chama hicho kinaweza kuwa makazi ya baadhi ya viongozi wakuu wanaojipanga kwa uchaguzi wa 2027.
Seneta huyo ni mmoja wa wanasiasa waliojitokeza hadharani kuunga mkono azma ya kisiasa ya Bw Sifuna.
Mbunge wa Saboti Caleb Amisi pia amesajili chama cha People’s Renaissance Movement (PM).
Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa Linda Mwananchi wanasemekana kuwa na mashaka kuhusu kutumia chama hicho licha ya Bw Amisi kuwa sehemu ya vuguvugu hilo.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi amethibitisha kuwa kundi hilo lina chaguo kadhaa mezani lakini akakataa kutaja majina.
Alisema kufanya hivyo mapema kunaweza kuvuruga mipango yao kutokana na kile alichodai kuwa hujuma za kisiasa kutoka kwa wapinzani wao.
“Linda Mwananchi ni chapa ambayo sisi tumejenga na kuvumisha. Wakenya wanaijua na wanaifahamu vizuri. Lakini hata kama tutanyimwa kuitumia, bado tuna njia nyingi za kuendelea mbele,” alisema Osotsi.
Kwa mujibu wake, kinachovutia wananchi si jina la chama bali sera, viongozi na maono ya vuguvugu hilo. Alisisitiza kuwa wafuasi wao wataendelea kuwaunga mkono hata wakishiriki uchaguzi kwa jina tofauti.
Mbali na changamoto za jina, kundi hilo pia linakimbizana na muda wa kutimiza masharti yaliyowekwa na IEBC.
Tume hiyo imeweka Oktoba 15, 2026 kuwa tarehe ya mwisho kwa vyama vya siasa kuwasilisha majina ya maafisa wake walioidhinishwa pamoja na sahihi zao rasmi kwa maandalizi ya uchaguzi wa 2027.
IEBC pia imepanga Oktoba 30 kuwa tarehe ya kuthibitisha kanuni za uteuzi wa vyama vya kisiasa, huku vyama vikitarajiwa kuwasilisha kanuni hizo ifikapo Novemba 6.
Katika maelezo yaliyowasilishwa mbele ya mahakama, viongozi wa Linda Mwananchi walisema kufikia Agosti 13, 2026, jukwaa lao la kidijitali lilikuwa na wanachama zaidi ya 55,000 waliojisajili wenyewe pamoja na zaidi ya 13,000 wa kujitolea.