Shule ya Msingi Madenge wajengewa uzio
DAR ES SALAAM; MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Madenge, Temeke, Dar es Salaam, Khadija Mani ameishukuru Jubilee Group kwa kuwajengea ukuta kuzunguka shule hiyo kwa lengo la kuimarisha usalama na kuondoa changamoto ya usumbufu uliokuwa ukisababishwa na wapita njia na kuathiri mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Akizunguka katika hafla ya makabidhiano ya ukuta huo, …
DAR ES SALAAM; MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Madenge, Temeke, Dar es Salaam, Khadija Mani ameishukuru Jubilee Group kwa kuwajengea ukuta kuzunguka shule hiyo kwa lengo la kuimarisha usalama na kuondoa changamoto ya usumbufu uliokuwa ukisababishwa na wapita njia na kuathiri mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Akizunguka katika hafla ya makabidhiano ya ukuta huo, Mwalimu Khadija alisema kwa sasa shule inanufaika na mazingira salama na tulivu yanyowawezesha walimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, huku wanafunzi wakipata mazingira bora ya kujifunza na kufanya vizuri kitaaluma.
“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Jubilee Life Insurance kwa kuijengea shule yetu uzio katika upande uliokuwa na changamoto kubwa. Hapo awali hatusoma kwa utulivu kutokana na usumbufu uliokuwa ukitokea mara kwa mara,” alisema.
Aliongeza kuwa ujenzi wa uzio huo umerejesha utulivu na usalama shuleni, huku ukiondoa kabisa vitendo vya usumbufu kutoka kwa wapita njia na watu waliokuwa wakivamia eneo la shule.
Naye Mkurugenzi wa Jubilee Group Tanzania Dk Harold Adamson alisema wanaamini kuwa ukuta huu utachangia kuimarisha mazingira salama na tulivu ya elimu, hivyo kuwapa walimu nafasi bora ya kufundisha wanafunzi katika mazingira mazuri bora.
Alisisisitiza kuwa Jubilee Group itaendelea kutekeleza shughuli za uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwa lengo la kuchangia maendeleo katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii, kwa kuamini kuwa jamii yenye maendeleo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.
Aidha Jubilee Life Insurance imechangia pia kuboresha mazingira ya shule kwa kupanda miti iliyosaidia kuhifadhi mazingira, imeipatia shule vifaa vya usafi, ikiwemo reki, majembe na fyekeo, ambavyo vinaendelea kusaidia kutunza usafi wa mazingira ya shule kila siku.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na MaOfisa Watendaji Wakuu wa Jubilee Life Insurance na Jubilee Health Insurance, Helena Mzena pamoja na viongozi wa serikali za mitaa, uongozi wa shule na wafanyakazi wa Jubilee Group Tanzania.