Shigella: Wakurugenzi mtabeba gharama za intaneti ofisini

Habari Leo
Published: May 02, 2026 08:14:58 EAT   |  General

GEITA: MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ameagiza waajiri ikiwemo wakurugenzi wa halmashauri kugharamia huduma ya intaneti kwa watumishi ili kufanikisha utendaji bora pasipo kuhusisha gharama binafsi za watumishi. Shigela ametoa maagizo hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi, 2026) ambapo kwa mkoa wa Geita yalifanyika katika Mamlaka ya Mji Mdogo …

The post Shigella: Wakurugenzi mtabeba gharama za intaneti ofisini first appeared on HabariLeo.

GEITA: MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ameagiza waajiri ikiwemo wakurugenzi wa halmashauri kugharamia huduma ya intaneti kwa watumishi ili kufanikisha utendaji bora pasipo kuhusisha gharama binafsi za watumishi.

Shigela ametoa maagizo hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi, 2026) ambapo kwa mkoa wa Geita yalifanyika katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro halmashauri ya wilaya ya Geita.

Kauli hiyo inakuja kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mkoani Geita ambapo walidai kuwa watumishi wanalazimika kutumia pesa binafsi kugharamia intaneti.

Shigela amesema ni wajibu wa waajiri kuweka mazingira rafiki kwa watumishi wao kufanya kazi bila kikwazo ambapo katika kipindi hiki cha matumizi makubwa ya TEHAMA suala la intaneti ni moja ya hitaji la msingi.

 

“Ni hoja ya msingi, waajiri tunao wajibu wa kuliangalia jambo hili na hususani wakurugenzi ndio mna wafanyakazi wengi wanaohitaji vifurushi vya intaneti, kwa hiyo kwenye mapato yenu ya ndani angalieni”, amesema.

Shigela amewataka wakuu wa shule na wakuu wa Idara ya afya kutuma taarifa ya gharama za intaneti maofisini kila mwezi ama kila robo mwaka ili hatua za haraka zichukuliwe kutoa malipo kulingana na matumizi.

Amesema serikali inaendelea kuboresha huduma ya mawasiliano kwenye maeneo yote ikiwemo yale yenye kasi ndogo ya intaneti ili kuwasaidia watumishi wa sekta za umma na binafsi kufanya kazi kwa ufasaha.

Aidha ameitaka TUCTA kuwasilisha taarifa ya taasisi zote ambazo zimeshindwa kukidhi matakwa ya kima cha chini na kutekeleza takwa la kisheria la uwasilishaji wa fedha za mifuko ya kijamii ili zichukuliwe hatua.

Akizungumza kwa niaba ya TUCTA, Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Geita, Pauline Tinda amesema wafanyakazi wengi wanalazimika kutumia gharama binafsi kulipia bando la intaneti.

Tinda amesema changamoto hiyo inatokana na kutozingatiwa kwa malipo na stahiki za kazi za ziada kwa watumishi wa umma jambo ambalo serikali inapaswa kulifanyia kazi ili kuwapunguzia mzigo watumishi.

The post Shigella: Wakurugenzi mtabeba gharama za intaneti ofisini first appeared on HabariLeo.