Serikali yaongeza bajeti mikopo elimu ya juu

Katika kipindi cha miaka minne, bajeti ya mikopo ya elimu imepanda kutoka shs bilioni 464 (2020/2021) hadi shs bilioni 787 (2024/2025). Kwa mwaka mpya wa masomo wa 2025/2026, bajeti iliyoidhinishwa imefikia shs bilioni 916.7, ikiwa ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuwekeza zaidi katika elimu. Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. …
Katika kipindi cha miaka minne, bajeti ya mikopo ya elimu imepanda kutoka shs bilioni 464 (2020/2021) hadi shs bilioni 787 (2024/2025).
Kwa mwaka mpya wa masomo wa 2025/2026, bajeti iliyoidhinishwa imefikia shs bilioni 916.7, ikiwa ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuwekeza zaidi katika elimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema hayo leo Juni 06, 2025 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Miongozo ya Uombaji Mikopo.
Amesema kuongezeka kwa bajeti kumewezesha idadi ya wanufaika wa mikopo kupanda kutoka 145,000 mwaka 2020/2021 hadi 245,799 mwaka 2024/2025.
Katika mwaka 2025/2026, wanafunzi 252,773 wanatarajiwa kunufaika, wakiwemo wanafunzi 88,320 wa mwaka wa kwanza, huku wengine 164,453 wakiendelea na masomo yao.
Prof. Nombo ameongeza kuwa Serikali pia imeendelea kuimarisha programu ya Samia Skolashipu, ambayo imewanufaisha wanafunzi wa Shahada za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Afya, ikiwakilishwa na shs bilioni 16.8 kwa wanafunzi 3,186 wa shahada za awali na 80 wa shahada ya umahiri.
Aidha, Serikali imepanua utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya Stashahada, ambapo wanafunzi 18,000 wanatarajiwa kupangiwa mikopo yenye thamani ya shs bilioni 64 kwa masomo ya kipaumbele kama Tiba, Ualimu, Madini, Usafirishaji, Uhandisi wa Nishati na Kilimo.
“Ili kuboresha huduma za upangaji na uombaji wa mikopo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeunganisha mifumo yake na wadau muhimu kama NECTA, TCU, NIDA, RITA, TASAF na wengine, kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu,” amesema Prof. Nombo.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuonyesha dhamira yake katika kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa bora za elimu kwa kupitia uwekezaji huo mkubwa wa fedha katika sekta ya elimu.