Serikali yaimarisha ubunifu, utafiti elimu ya juu

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kutekeleza mikakati endelevu ili kuwapa fursa viongozi wapya na wabobezi kuonesha uwezo na ubunifu katika taasisi za elimu ya juu. Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne …
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kutekeleza mikakati endelevu ili kuwapa fursa viongozi wapya na wabobezi kuonesha uwezo na ubunifu katika taasisi za elimu ya juu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema mikakati hiyo inajumuisha kuongeza ufadhili wa utafiti na uvumbuzi kupitia Mfuko wa Taifa wa Utafiti na Uvumbuzi (TTIF).
Aidha, amesema imeanzishwa na kuimarishwa vituo vya Ubunifu (Innovation Hubs) katika vyuo vikuu ili kuhimiza ubunifu wa kibiashara na kufadhili miradi ya wanafunzi na wahadhiri.
Prof. Nombo ameeleza kuwa Wizara imechukua hatua za kuboresha mafunzo ya walimu wa vyuo vikuu kwa kuimarisha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji, hususan kwa matumizi ya teknolojia na elimu pepe (e-learning).
Wizara pia inashirikiana na wadau wa ndani na kimataifa, kama Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa, ili kuongeza vyanzo vya ufadhili na maarifa ya ziada.
Mfumo wa uhakiki ubora wa elimu kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) umeendelea kuimarishwa kwa lengo la kuongeza vigezo vya kimataifa kwa programu za masomo.
Prof. Nombo amesema Wizara inaendelea kutekeleza Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wenye lengo la kuboresha mfumo wa usimamizi na mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kuendana na ajenda ya maendeleo ya nchi.
Hatua hizo zinatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ya juu nchini kwa kuhakikisha kuwa taasisi za elimu zinazalisha wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya maendeleo na ushindani wa kimataifa.