Samia: Mradi wa urani usiwasahau wananchi Namtumbo

Habari Leo
Published: Jul 30, 2025 19:32:12 EAT   |  Jobs and Career

RUVUMA:RAIS Samia Suluhu Hassan, ameitaka kampuni ya Mantra Tanzania inayosimamia mradi wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya urani wilayani Namtumbo kuhakikisha inazingatia wajibu wake kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR) na ushirikishwaji wa Watanzania katika ajira na shughuli zote za kiuzalishaji. Akizungumza na wananchi wa Namtumbo mkoani Ruvuma mara baada ya kuzindua rasmi …

RUVUMA:RAIS Samia Suluhu Hassan, ameitaka kampuni ya Mantra Tanzania inayosimamia mradi wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya urani wilayani Namtumbo kuhakikisha inazingatia wajibu wake kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR) na ushirikishwaji wa Watanzania katika ajira na shughuli zote za kiuzalishaji.

Akizungumza na wananchi wa Namtumbo mkoani Ruvuma mara baada ya kuzindua rasmi kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa urani, Rais Samia amesema kuwa manufaa ya mradi huo yanapaswa kuwagusa moja kwa moja wakazi wa maeneo ya jirani kwa kupewa kipaumbele katika ajira zisizohitaji ujuzi maalum.

Kwa mujibu wa Rais, mradi huo wa kimkakati unaotekelezwa katika Bonde la Mto Mkuju unatarajiwa kuwa na maisha ya uzalishaji ya zaidi ya miaka 20, na unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa taifa na jamii inayouzunguka.

Rais Samia amesema mradi huo umeonesha jitihada za serikali katika kuongeza thamani ya rasilimali za taifa na kuchochea ajira kwa Watanzania, lakini amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wa Namtumbo na maeneo ya jirani wananufaika moja kwa moja.