Samia: EACLC itachochea ufanisi Bandari Dar

DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa uzinduzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato ya serikali, ajira kwa vijana, na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichopo …
DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa uzinduzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato ya serikali, ajira kwa vijana, na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichopo Ubungo, Dar es Salaam leo Agosti mosi, 2025 Rais Samia amesema mradi huo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya biashara na usafirishaji, hasa kwa kuchochea mauzo ya nje na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.
Amebainisha kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama kitovu cha biashara na usafirishaji kwa nchi zote za Afrika Mashariki kwa kuwaunganisha wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na walaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Pia amesema eneo hilo lina maghala ya kisasa, ofisi za biashara, na huduma zote muhimu za usafirishaji zilizo katika sehemu moja, hatua itakayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama na muda wa kusafirisha mizigo.
Rais Samia pia ameeleza kuwa mradi huo unaendana na mkakati wa serikali wa kujenga uchumi wa kidijitali, kwani shughuli nyingi katika kituo hicho zitasimamiwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kielektroniki.
Mradi wa EACLC ulianza kutekelezwa mwezi Mei mwaka 2023 na hadi kukamilika kwake umetajwa kugharimu Sh bilioni 282.7, serikali inatarajia kituo hicho kitaiweka Tanzania kwenye nafasi ya kwanza kama kitovu cha biashara kwa Afrika Mashariki na Kati.