PPP, REDET kufanya kongamano Dira 2050 Mwanza

Habari Leo
Published: Jul 25, 2025 17:48:57 EAT   |  Educational

MWANZA: Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kinatarajiwa kufanya kongamano la kitaaluma kesho mkoani Mwanza, linalolenga kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050. Mkuu wa Idara ya …

MWANZA: Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kinatarajiwa kufanya kongamano la kitaaluma kesho mkoani Mwanza, linalolenga kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Lupa Ramadhani amesema leo Julai 25,2025 kwamba kongamano hilo ni hatua ya awali katika utekelezaji wa dira hiyo, likilenga pia kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi katika mijadala ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji wa pamoja katika kujenga taifa.

Amerejea tukio la Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua dira hiyo wiki iliyopita, akisema msisitizo umewekwa katika nafasi ya ubia kutokana na malengo yake (Dira) kuhimiza ushiriki wa kila mtanzania katika kuleta maendeleo ya nchi, lakini vilevile kuzingatia uwazi na utawala bora.

“Hivyo kongamano hili lina umuhimu wa kimkakati kwa sababu linatoa fursa ya kuchambua nafasi ya ubia katika sekta za umma na binafasi juu ya kuleta maendeleo ya taifa,” amesema.

Imefahamika zaidi kwamba idadi ya washiriki inatarajiwa kuwa 300 wa kada mbalimbali, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, taasisi binafsi , vijana , wanawake na wasomi.

Mkuu wa Kitengo cha Habari PPP, Chelu Matuzya, amesistiza kuwa kongamano lina mlengo wa kujadiliana kwa uwazi ubia ,uwekezaji, na mwenendo wa kiuchumi katika miaka 25 ijayo, hatimaye kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa si tu kwa wakati, bali kwa viwango vya ubora vinaotakiwa.