Pongezi EALA kutaka kilimo cha ikolojia

MWISHONI mwa wiki Bunge la Jumuiya wa Afrika Mashariki (EALA) lilikutana kujadili na kupitisha ripoti ya kamati za kilimo, maliasili na utalii kuhusu kilimo cha ikolojia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kwa mujibu wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kilimo cha ikolojia ni mbinu ya kilimo inayotumia maarifa na kanuni …
MWISHONI mwa wiki Bunge la Jumuiya wa Afrika Mashariki (EALA) lilikutana kujadili na kupitisha ripoti ya kamati za kilimo, maliasili na utalii kuhusu kilimo cha ikolojia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kwa mujibu wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kilimo cha ikolojia ni mbinu ya kilimo inayotumia maarifa na kanuni za jinsi mazingira asili hufanya kazi (ikolojia) kwa muundo na usimamizi wa kilimo ikimaanisha na maumbile asili na kudhibiti maingiliano yenye faida kati ya mimea, wadudu na vijidudu vya udongo.
Mbinu hiyo inahitaji bidii na maarifa lakini inaweza kuwa yenye tija kuchangia katika maisha endelevu na usalama wa chakula cha nyumbani kwa kutoa mapato anuwai kila mwaka.
Misingi ya kilimo cha ikolojia ni kilimo cha misitu, kilimo cha viwanda, ukulima wa mmea wa aina moja na pembejeo.
Eala ilijadili hilo baada ya semina waliyopata kuhusu kilimo cha ikolojia iliyofanyika Kampala, Uganda kuanzia Novemba 13 -15, 2024. Semina hiyo iliratibiwa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na Kituo cha Haki za Chakula na Maisha Bora (CEFROHT).
Mbali na wabunge wa Eala wengine walioshiriki kwenye semina hiyo ni wakulima, watafiti na washirika wa maendeleo.
Wabunge hao waliazimia kuingizwa kwa sera ya kilimo cha ikolojia kwa nchi za EAC ili kukuza mifumo ya chakula endelevu, yenye ustahimilivu na usawa katika jumuiya hiyo na kulitaka baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo kulifanyia kazi suala hilo.
Kwa mujibu wa Eala ikolojia siyo mbinu ya kilimo bali ni harakati ya mabadiliko muhimu katika kushughulikia upotevu wa utofauti wa viumbe, mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa udongo, na uhaba wa chakula, suala linaloathiri mamilioni ya watu duniani kote.
Kutokana na umuhimu wa kilimo hicho, Eala imetaka kuandaliwa kwa sheria za kikanda zinazokuza mbinu za kilimo endelevu na kuongeza usalama wa chakula, kuimarisha sera za kulinda mifumo ya mbegu za kienyeji na mila za chakula za jadi, kuhakikisha uhuru wa chakula, kuongeza rasilimali kwa ajili ya utafiti wa kilimo cha ikolojia, benki za mbegu za jamii, na mbinu bunifu za kilimo.
Kuwezesha wanawake, vijana na makundi yaliyo katika hatari kuwa wakongwe wa maendeleo ya kilimo cha ikolojia na mabadiliko ya mifumo ya chakula, kuanzisha benki za mbegu za jamii, kuunga mkono usambazaji wa maarifa ya kilimo cha ikolojia kupitia majukwaa mbalimbali na kukuza juhudi za wakulima na masoko yanayoongozwa na wakulima.
Tunaunga mkono ushauri huo wa Eala na tunaamini utafanyiwa kazi kwani kwa hali ilivyo sasa hakuna budi kufanya kilimo hicho kwa manufaa ya nchi husika kwani itasaidia kukuza uchumi wa wananchi na nchi kwa ujumla na hatimaye EAC kunufaika.
Athari za mabadiliko ya tabianchi zipo duniani kote hivyo ni vyema kwa nchi za EAC kutumia watalamu wake wa kilimo na kukitambulisha kilimo cha ikolojia kwa wananchi wake ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko hayo.