Oburu angali Uingereza, asubiri madaktari wampe idhini kurejea
KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, bado yuko nchini Uingereza akipokea matibabu huku familia yake ikisema hali yake imeimarika lakini bado hajaruhusiwa na madaktari kurejea nchini.
Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga, ambaye ni dadake mdogo, alisema mwanasiasa huyo mkongwe anaendelea kufuatiliwa na madaktari na familia haijafanya mipango yoyote ya haraka ya kumrejesha nyumbani.
Kwa mujibu wa Bi Odinga, jambo la msingi kwa sasa ni kuruhusu madaktari kukamilisha kukagua afya yake kabla ya uamuzi wowote kufanywa kuhusu safari yake ya kurejea Kenya.
“Ameimarika sana, lakini hatujapanga kurejea kwake Kenya kwa sasa,” alisema Bi Odinga akiwa Uingereza.
Aliongeza kuwa familia haina haraka ya kumrejesha nchini kwa kuwa bado ana miadi kadhaa ya matabibu ambayo lazima ahudhurie.
Bi Odinga alifafanua kuwa Dkt Oginga hajalazwa hospitalini kwa sasa. Badala yake, anaishi karibu na hospitali anayohudumiwa ili iwe rahisi kuhudhuria ukaguzi na miadi ya madaktari.
“Hajalazwa. Tunaishi karibu na hospitali, kwa hivyo ni rahisi kwake kuonana na madaktari wakati wowote anapohitajika,” alisema.
Familia hiyo imesisitiza kuwa afya ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 83 ni muhimu zaidi kuliko majukumu yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, hawataki kuharakisha kurejea kwake kabla madaktari kuthibitisha kuwa yuko katika hali nzuri.
Habari hizo zinajiri huku Dkt Oginga akiendelea kushiriki shughuli mbalimbali kwa njia ya mtandao akiwa Uingereza. Wiki hii alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akieleza kuwa yeye na mkewe, Mama Judy, walimpokea Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Maurice Makoloo, katika makazi yao.
Alisema walijadili jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na Uingereza, kusaidia Wakenya wanaoishi ughaibuni pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji na ujuzi wao.