Nyang’hwale mguu sawa kupokea kidato cha kwanza

Habari Leo
Published: Jan 09, 2026 15:59:48 EAT   |  Educational

GEITA: HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita imeweka wazi kuwa imeandaa miundombinu inayotosheleza kupokea wanafunzi 3,056 wa kidato cha kwanza mwaka 2026. Ofisa Elimu Sekondari wilayani Nyang’hwale, Malemu Tito ametoa taarifa hiyo katika ziara ya mkuu wa wilaya kukagua miundombinu ya elimu kuelekea mwaka mpya wa masomo. Malemu amesema mpaka sasa tathimini inaonyesha kuwa …

The post Nyang’hwale mguu sawa kupokea kidato cha kwanza first appeared on HabariLeo.

GEITA: HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita imeweka wazi kuwa imeandaa miundombinu inayotosheleza kupokea wanafunzi 3,056 wa kidato cha kwanza mwaka 2026.

Ofisa Elimu Sekondari wilayani Nyang’hwale, Malemu Tito ametoa taarifa hiyo katika ziara ya mkuu wa wilaya kukagua miundombinu ya elimu kuelekea mwaka mpya wa masomo.

Malemu amesema mpaka sasa tathimini inaonyesha kuwa halmashauri hiyo haina upungufu wa vyumba vya madarasa kwenye shule zote za sekondari hivo kila mwanafunzi atapokelewa.

Amesema ukaguzi uliofanyika umebaini bado kuna upungufu mdogo wa meza pamoja na viti vya wanafunzi ambapo juhudi zinaendelea kuziba pengo kabla ya shule kufunguliwa.

“Matarajio ni kwamba kufikia siku ya kufungua shule upungufu uliopo utakuwa umefanyiwa kazi kwa maana kwamba tunatarajia kutengeneza viti na meza”, amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Ezekiel Ntiriyo amesema maagizo yameshatolewa kwa wakuu wa shule kusimamia ukarabati wa viti na meza vilivyoharibika.

“Wakuu wa shule huwa wanatengewa bajeti ya ukarabati na matengenezo ya miundombinu watazitumia hizo pesa kutengeneza meza, viti na madawati yaweze kurejea kwenye matumizi”.

Amesema pia maagizo yametolewa kwa kamati za maendeleo ngazi ya kata kushirikisha wadau wa maendeleo kufanya tathimini ya viti, meza na madawati na kuangalia namna ya kutatua tatizo.

Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame amesema tayari amefanya ukaguzi kwenye shule zote 19 za sekondari lengo kuu likiwa ni kujiridhisha utayari wa wilaya kupokea watoto.

Amesema ili kukabiliana na upungufu meza na viti halmashauri imejipanga kutenga kiasi kidogo cha pesa kila mwezi kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kufanya matengenezo na ukarabati.

“Maelekezo ya serikali ni kuhakikisha kila mtoto anakwenda darasani, kuanzia shule ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza”, alisema na kuongeza;

“Tunatamani kuona Nyang’hwale inakuwa kinara kwenye elimu, kwa sababu kipaumbele cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na kipaumbele cha tatu ni elimu”.

The post Nyang’hwale mguu sawa kupokea kidato cha kwanza first appeared on HabariLeo.