Nyagawa awapa motisha wahitimu wa Lugalo Sekondari

IRINGA: Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Charles Nyagawa, amewataka wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Lugalo kutanguliza Mungu katika masomo na maisha yao, huku akiwahakikishia motisha ya kupata usafiri wa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha endapo watafanya vizuri katika mitihani yao ya taifa. Nyagawa aliyasema hayo …
The post Nyagawa awapa motisha wahitimu wa Lugalo Sekondari first appeared on HabariLeo.
IRINGA: Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Charles Nyagawa, amewataka wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Lugalo kutanguliza Mungu katika masomo na maisha yao, huku akiwahakikishia motisha ya kupata usafiri wa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha endapo watafanya vizuri katika mitihani yao ya taifa.
Nyagawa aliyasema hayo leo wakati wa mahafali ya 57 ya kidato cha nne katika shule hiyo, ambapo jumla ya wanafunzi 131—wavulana 77 na wasichana 54—walihitimu masomo yao baada ya safari ya miaka minne.
“Mkitanguliza Mungu, mtavuna matokeo mazuri. Wanadamu tunaangamia kwa kukosa maarifa, hivyo jiepusheni na magenge yatakayohatarisha ndoto zenu. Akili zenu ziwe za kufika chuo kikuu, nyinyi ni viongozi wa Taifa la kesho,” alisema Nyagawa, huku akiwataka wahitimu wasiruhusu ndoto zao kufa mapema.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Lugalo, PrayGod Makongwa, alisema mafanikio ya shule hiyo yamechochewa na sera ya elimu bure pamoja na maboresho ya miundombinu.
Alibainisha kuwa zaidi ya Sh Milioni 130 zimepokelewa shuleni hapo kwa ajili ya ujenzi kwa bweni jipya, na Sh milioni 55 zimepokeleqa kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa bweni lingine.
Makongwa alisema lengo la mabweni hayo ni kuongeza nafasi za wasichana kupata elimu katika mazingira bora na salama.
Shule kwa sasa ina wanafunzi 1,007, wakiwemo wasichana 707, ambapo kati yao 402 wanakaa bweni.
“Lugalo tunataka kusahau daraja sifuri, sasa tunataka matokeo ya daraja la kwanza na la pili pekee. Ndiyo dira yetu kwa wahitimu hawa,” alisema Makongwa.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, wahitimu Grace Massengo na Henry Mbaga walisema safari yao haikuwa rahisi kwani walianza 160 lakini wanaomaliza ni 131.
Walipongeza walimu kwa kuwalea kwa nidhamu na ujuzi, huku wakiahidi kuwa matokeo ya mwaka huu yatakuwa mazuri zaidi.
Hata hivyo, walitaja changamoto zinazoikabili shule ikiwemo uhaba wa fedha za kukamilisha mabweni, miundombinu mibovu ya michezo, ukosefu wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, ukuta wa usalama wenye urefu wa mita 50 uliobomoka, nyumba ya mwalimu iliyoungua moto pamoja na uhaba wa vifaa vya TEHAMA kama printer za kuchapisha mitihani.
“Tunawaomba wadau na serikali kutusaidia kupunguza changamoto hizi ambazo zikiratibiwa vizuri zitaongeza ufaulu na usalama wa wanafunzi, hususan wasichana,” walisema.
Katika harambee iliyofanyika wakati wa mahafali, wazazi na wadau waliweza kuchangia Sh 1,876,500 na mifuko 30 ya saruji. Miongoni mwa wachangiaji wakubwa alikuwa Mama Ester Shambe, aliyetoa mifuko ya saruji, na Mwalimu Aman Felix ambaye aliongoza ukarabati wa nyumba ya walimu iliyoungua moto.
The post Nyagawa awapa motisha wahitimu wa Lugalo Sekondari first appeared on HabariLeo.