Ngupula: Ninajua ‘Password’ ya changamoto barabara Mufindi Kaskazini

Habari Leo
Published: Aug 02, 2025 10:51:28 EAT   |  News

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Godfrey Ngupula, ameendelea na kampeni zake katika kata mbalimbali za jimbo hilo akiahidi kushughulikia changamoto ya barabara inayolalamikiwa kwa muda mrefu, huku akisema jimbo hilo limekosa mtu mwenye “neno la siri” au ‘password’ ya kufanikisha ufumbuzi wake. Akizungumza katika mikutano yake ya …

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Godfrey Ngupula, ameendelea na kampeni zake katika kata mbalimbali za jimbo hilo akiahidi kushughulikia changamoto ya barabara inayolalamikiwa kwa muda mrefu, huku akisema jimbo hilo limekosa mtu mwenye “neno la siri” au ‘password’ ya kufanikisha ufumbuzi wake.

Akizungumza katika mikutano yake ya kampeni, Ngupula alisema barabara muhimu ikiwemo ile ya Mdabulo na ile ya Kinyanambo hadi Madibira, zimeendelea kuwa kero kwa wananchi, hali inayokwamisha maendeleo.

“Changamoto kubwa katika jimbo hili ni barabara. Mimi ni mtu mwenye password, nipeni ridhaa tupate lami,” alisema Ngupula

Ngupula, ambaye katika kura za maoni za mwaka 2020 alishika nafasi ya pili, alisema uzoefu wake wa uongozi ni chachu ya kutatua changamoto hizo, akitaja sifa tatu kuu za kiongozi alizonazo kuwa ni upendo, uwezo wa kutekeleza mambo magumu na ustahimilivu.

“Zote hizo ninazo, na nina hakika zikipewa nafasi zitabadili hali ya maendeleo jimboni,” alisema.

Mbali na uzoefu wa kushika nyadhifa serikalini ikiwemo kuwa Mkuu wa Wilaya, Ngupula kwa sasa ni Mhifadhi Mkuu wa Bahari katika hifadhi za bahari na maeneo tengefu nafasi anayosema imemjengea uwezo wa kupanga na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo.

Amesema iwapo atapata ridhaa ya wananchi kupitia kura za maoni ndani ya CCM na baadaye uchaguzi mkuu, ataweka kipaumbele kwenye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kuboresha huduma za kijamii na kuhamasisha miradi ya uchumi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.