Ndejembi: Uwekezaji elimu ya juu ulete matokeo
IRINGA: Ujenzi wa maabara za kisasa, hosteli, maktaba na majengo ya kitaaluma wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 30.4 katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) unatarajiwa kuongeza uwezo wa chuo hicho kuandaa walimu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta ya elimu. Aidha, Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi wa fedha na ukamilishaji wa miradi kwa …
IRINGA: Ujenzi wa maabara za kisasa, hosteli, maktaba na majengo ya kitaaluma wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 30.4 katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) unatarajiwa kuongeza uwezo wa chuo hicho kuandaa walimu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta ya elimu.
Aidha, Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi wa fedha na ukamilishaji wa miradi kwa wakati.
Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi, amesema kila shilingi inayowekezwa katika elimu ya juu lazima ilete matokeo yanayopimika kwa wananchi, akiuagiza uongozi wa chuo hicho kusimamia kwa umakini, uwazi na uadilifu fedha za miradi ya maendeleo.
Ndejembi alitoa msisitizo huo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo mapya ya MUCE mkoani Iringa, akieleza kuwa Serikali inalenga kupanua fursa za elimu ya juu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa.
Amesema Serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imewekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 425, sawa na takribani Sh trilioni moja, kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaolenga kuimarisha miundombinu na ubora wa elimu ya juu nchini.
“Ni muhimu fedha hizi zisimamiwe kwa uwazi na uadilifu, miradi ikamilike kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora. Serikali haitavumilia matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma,” amesisitiza.
Amesema uwekezaji katika elimu unapaswa kuendana na ongezeko la wahitimu wa elimu ya msingi na sekondari, ili vijana wengi zaidi wapate nafasi za kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kupata ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesema Mkoa wa Iringa umepokea zaidi ya Sh bilioni 175 tangu mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika ngazi mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema uwekezaji kupitia HEET umeimarisha mazingira ya ufundishaji, ujifunzaji, utafiti na ubunifu katika taasisi za elimu ya juu nchini.
Amesema jumla ya taasisi 20 za elimu ya juu zimenufaika na ujenzi wa maabara 309, hosteli 26, pamoja na maktaba, mikahawa na ofisi 1,177, huku majengo 48 yakifanyiwa ukarabati.
Profesa Mkenda amesema juhudi hizo zinaenda sambamba na upanuzi wa upatikanaji wa elimu ya juu kupitia kampasi mpya katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kupunguza changamoto za umbali na gharama za masomo kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete, amesema MUCE inaendelea kuimarisha miundombinu yake kupitia miradi saba yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 30.4.
Amesema miradi hiyo inajumuisha majengo ya sayansi, maabara ya fizikia, majengo ya midia anuwai na elimu maalumu, hosteli za wanafunzi pamoja na maktaba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Dk Kikwete, hadi Septemba 30, 2026, majengo manne yanayofadhiliwa kupitia HEET yalikuwa yamekamilika kwa asilimia 100.
Uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa MUCE kudahili wanafunzi wengi zaidi na kuboresha mafunzo ya vitendo, hususan katika maandalizi ya walimu wa sayansi na masomo mengine.