Ndejembi: Umeme chachu maendeleo ya kiuchumi
DAR ES SALAAM: MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amesema Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, utarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa mijini na vijijini na kuongeza fursa za maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Akizungumza leo Oktoba 2, …
DAR ES SALAAM: MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amesema Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, utarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa mijini na vijijini na kuongeza fursa za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza leo Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini na uzinduzi wa mpango huo, Ndejembi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Misheni 300, unaolenga kuhakikisha hadi mwaka 2030 wananchi milioni 300 barani Afrika wanafikiwa na nishati ya umeme.
Amesema kupitia mpango huo, wananchi wanaostahili watanufaika na utaratibu wa kugharamiwa gharama za uunganishaji umeme, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya kufikisha huduma hiyo kwa kaya takribani milioni 1.7 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Nishati (National Energy Compact).
“Ninaipongeza TANESCO na Benki ya CRDB kwa hatua hii muhimu ya kuanzisha ushirikiano unaolenga kumrahisishia mwananchi kupata huduma ya umeme. Ushirikiano huu ni mfano bora wa namna taasisi za umma na sekta binafsi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali ili kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja,” amesema Ndejembi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dk. Juma Homera, amesema ushirikiano huo kati ya Serikali na sekta binafsi utawezesha wananchi kunufaika zaidi na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Balozi Zuhura Bundala, amesema mpango huo unaakisi juhudi za Serikali katika kuweka mazingira wezeshi ya kukuza fursa za kiuchumi na kijamii kupitia nishati ya umeme.
“Tunatarajia mpango huu uweze kuwafikia wananchi wengi, ambao tunaamini watanufaika na fursa mbalimbali ikiwemo ajira, uzalishaji, biashara na kuwezesha mazingira bora katika sekta ya elimu,” amesema Balozi Bundala.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema awamu ya kwanza ya mpango huo inalenga maeneo ya vijijini, ambapo Benki ya CRDB itawezesha Sh27,000 kwa kila kaya inayostahili, fedha ambazo zitalipwa moja kwa moja kwa TANESCO kama gharama za uunganishaji umeme bila mwananchi kuwa na wajibu wa kuzirejesha.
Amesema kwa wananchi wa mijini na pembezoni mwa miji, CRDB itawezesha upatikanaji wa fedha kupitia mikopo nafuu, ambayo italipwa kwa utaratibu utakaowekwa na benki hiyo.
“Mpaka sasa TANESCO ina takribani wateja milioni 6.4, lakini kupitia mpango huu wa ushirikiano tunatarajia idadi ya wateja itaongezeka na kufikia lengo la kuunganisha kaya milioni 1.7 kwa mwaka,” amesema Twange.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imetenga Sh bilioni moja kila mwaka kwa ajili ya mpango huo na kwa kushirikiana na TANESCO itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutumia fursa hiyo katika kukuza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Kupitia Mpango wa Kitaifa wa Nishati, Tanzania inalenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme kutoka asilimia 78.4 hadi asilimia 100, huku kiwango cha wananchi waliounganishwa na umeme kikilenga kuongezeka kutoka asilimia 46 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030.