Mpango ataka vijana wafuga samaki wasaidiwe

Habari Leo
Published: Aug 01, 2025 19:12:02 EAT   |  Business

DODOMA — Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Ijumaa aliiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwawezesha vijana wanaojihusisha na ufugaji wa samaki kwa vizimba kupata mitaji mikubwa ili kukuza shughuli zao na kufikia masoko ya kimataifa. Aidha, aliitaka wizara hiyo kuanzisha kampeni madhubuti ya kuwatangaza vijana hao kupitia vyombo vya habari ili wawe mfano kwa …

DODOMA — Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Ijumaa aliiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwawezesha vijana wanaojihusisha na ufugaji wa samaki kwa vizimba kupata mitaji mikubwa ili kukuza shughuli zao na kufikia masoko ya kimataifa.

Aidha, aliitaka wizara hiyo kuanzisha kampeni madhubuti ya kuwatangaza vijana hao kupitia vyombo vya habari ili wawe mfano kwa vijana wengine waingie kwenye ajira binafsi.

Dk. Mpango alitoa maagizo hayo alipotembelea maonesho ya kilimo ya Nane Nane mkoani Dodoma, baada ya kusikiliza ushuhuda wa kikundi cha vijana tisa kutoka “Vijana Nguvu Kazi Mwanza” wanaojishughulisha na ufugaji wa samaki kwa vizimba kwa msaada wa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

“Vijana hawa nataka tuwaone mara kwa mara kwenye vyombo vya habari. Wapo vijana wengi mitaani wanalalamika kuhusu ajira. Tuwatumie hawa kama walimu kwa wengine ili wajiajiri kupitia ufugaji wa samaki,” alisema.

Kikundi hicho kilipata mkopo wa Sh milioni 137.9 kutoka TADB na kununua vizimba tisa, ambavyo vilisaidia kuanzisha ufugaji. Ndani ya miezi sita walivuna vizimba sita na kupata faida ya Sh milioni 102. Baada ya kuvuna vizimba vitatu vilivyobaki, walipata Sh milioni 25, wakaweza kurejesha mkopo wa Sh milioni 68 na kugawana Sh milioni 34 walizobakiwa nazo.

Baada ya kulipa mkopo huo, walipata mkopo mwingine wa Sh milioni 63 kutoka TADB na kufanikisha faida ya Sh milioni 106.

“Tunatamani kuanza kuchakata na kuuza samaki nje ya nchi. Tunaiomba serikali itusaidie kupata mtaji mkubwa zaidi kwa sababu faida tunayopata hugawanywa kwa watu tisa,” alisema Katibu wa kikundi hicho, Pius Makindi.

Aliongeza kuwa wakiwa na vizimba vingi, angalau 30 hadi 50, faida itakuwa kubwa zaidi na wataweza kuinuka kiuchumi haraka.

Dk. Mpango aliipongeza TADB kwa mchango wake kwa vijana na kusisitiza kuwa soko la minofu ya samaki ni kubwa ndani na nje ya nchi.

“Naipongeza sana TADB kwa kuwawezesha vijana hawa. Endeleeni kuwashika mkono ili waweze kukua zaidi,” alisema.