Miradi ya PPP yashika kasi

Habari Leo
Published: Feb 16, 2026 07:30:41 EAT   |  Business

UTEKELEZAJI wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 umewezesha kuanza utekelezaji wa miradi mitano ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP). Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027 yametaja miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa la biashara kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 14.8.

The post Miradi ya PPP yashika kasi first appeared on HabariLeo.

UTEKELEZAJI wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 umewezesha kuanza utekelezaji wa miradi mitano ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP). Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027 yametaja miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa la biashara kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 14.8.

Mapendekezo hayo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Mipango yameeleza mradi huo unatekelezwa na Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam. Mradi mwingine ni wa utoaji huduma za mabasi kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza.

Mradi huo unatekelezwa na Wakala ya Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 81.4. Mwingine ni utoaji huduma za mabasi kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili.

Mradi huo unatekelezwa na Dart kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 248.67. Mradi mwingine unaotekelezwa kwa PPP ni ujenzi wa barabara kipande cha kwanza kutoka KibahaMlandizi hadi Chalinze chenye urefu wa kilometa 78.9.

Ujenzi huo unatekelezwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 328. Mradi mwingine ni kuanzishwa kwa vituo vya ukaguzi wa magari unaotekelezwa na shirika la ujenzi la Jeshi la Polisi Tanzania kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 117.

Tume ya Taifa ya Mipango ilieleza katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imetekeleza miradi na programu zenye lengo la kutoa huduma, kuongeza ufanisi katika sekta za miundombinu na kuboresha mazingira ya biashara.

Imeeleza shughuli zilizotekelezwa katika kufikia malengo ya mpango ni pamoja na kuratibu majadiliano baina ya serikali na wawekezaji, kupata washauri elekezi kwa ajili ya ufunguaji wa kampuni na kufunguliwa kwa kampuni za uendeshaji.

Imetaja mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuanza kutekelezwa kwa miradi takribani mitano ya ubia, kuvutia uwekezaji kutoka nje, kuongeza mapato, kuongeza ajira na kusaidia uendelezaji wa sekta nyingine. “Aidha, sekta binafsi imeendelea kushirikiana na serikali ili kuwekeza katika miradi muhimu katika sekta za kilimo, viwanda, miundombinu, utalii ujenzi na mawasiliano,” imeeleza tume hiyo.

Uwekezaji na biashara Tume ya Taifa ya Mipango imeeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano ulilenga kurahisisha michakato ya uwekezaji na biashara, kupunguza gharama za uwekezaji na biashara, na kupunguza gharama za biashara kwa kuimarisha ufanisi. Imeeleza utekelezaji wa afua zilizowekwa umechangia kuongeza idadi ya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa kutoka 220 mwaka 2019/20 hadi 2,938 mwaka 2025/2026.

Kwa mujibu wa tume hiyo utekelelezaji waafua hizo umeongeza thamani ya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa kutoka Dola za Marekani milioni 1724.47 mwaka 2019/20 hadi Dola za Marekani milioni 11,267.29 mwaka 2024/2025.

Tume imeeleza utekelezaji huo umewezesha kuongezeka kwa ardhi ya uwekezaji iliyotengwa kutoka ekari 90,990 mwaka 2019/20 hadi 1,055,403 mwaka 2025/2026. Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027 yameeleza mafanikio yaliyopatikana yameongeza ushindani katika soko la ndani na nje, yameongeza uzalishaji viwandani na kuna ongezeko la uwekezaji nchini.

“Utekelezaji wa hatua madhubuti za uratibu na uhamasishaji pamoja na uendelezaji wa miundombinu wezeshi unaonesha kuwa chachu ya kuongezeka kwa usajili wa miradi mipya ya uwekezaji,” imeeleza Tume ya Taifa ya Mipango. SOMA: Ujumbe wa Burundi watua Dar kujifunza PPP-CENTRE

Imeeleza matarajio ya mwenendo wa sekta ni kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) na kuimarisha uhamasishaji na utekelezaji wa programu ya Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZ) ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya msingi ya ndani na kuzunguka maeneo husika.

Matarajio mengine ni kuainisha maeneo ya ardhi ya uwekezaji na kuweka mfumo madhubuti wa kisera, kisheria na kitaasisi wa kusimamia mashirika na taasisi za umma ili kuongeza tija katika uwekezaji wa umma ndani na nje ya nchi kwa kukamilisha utungaji wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma na Kanuni zake na kuanza uandaaji wa Sera ya Uwekezaji wa Umma.

The post Miradi ya PPP yashika kasi first appeared on HabariLeo.