Meneja Mkuu wa KCB Bank, Rosemary azikwa usiku kinyume na amri ya mahakama

Taifa Leo
Published: Aug 30, 2026 03:55:52 EAT   |  News

MZOZO kuhusu kifo cha Rosemary Chemutai Koech, meneja mkuu wa Benki ya KCB, na ‘umiliki’ wa mwili wake umechukua mkondo mpya baada ya familia yake kumzika usiku wa kuamkia Jumamosi licha ya amri ya mahakama iliyositisha mazishi hayo kwa muda. Rosemary, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha ulinzi wa data KCB, alifariki Agosti 21 akiwa na umri wa miaka 40 katika nyumba yake ya Ngong, Kaunti ya Kajiado. Kifo chake kilitokea alipokuwa amejitenga na mumewe, Kevin Migwe Kimwatu, kufuatia matatizo ya ndoa. Mapema Ijumaa, Mahakama ya Milimani jijini Nairobi iliamuru kwa muda mazishi yake kufanyika na ikazuia Lee Funeral Home kutoa mwili huo hadi kesi iliyowasilishwa na mumewe isikizwe na kuamuliwa. Hakimu Mkuu Mwandamizi Agnes Mwangi alitoa amri ya kuzuia wanafamilia, Lee Funeral Home na KCB kuhamisha mwili wa marehemu. Pia alisema mazishi yasifanyike bila idhini ya mume wa marehemu. Hata hivyo, mazishi yalifanyika saa saba na nusu usiku katika kijiji cha Chepseon, eneo la Kipkelion Mashariki, Kaunti ya Kericho. Akizungumza na waombolezaji Jumamosi, mwenyekiti wa ukoo Samwel Keter alisema familia iliamua kufanya hivyo kwa kuzingatia mila za Kalenjin. “Yanayosambazwa mitandaoni si ya kweli. Binti yetu alifariki na kwa mujibu wa utamaduni wetu, mtu wa aina hiyo hapaswi kukaa bila kuzikwa kwa zaidi ya siku tatu au nne. Pia, baada ya uchunguzi wa maiti kufanyika, mazishi yanapaswa kufanyika ndani ya siku mbili. Tulifanya tulichofanya kwa kuzingatia mila zetu ili tukio kama hilo lisijirudie,” alisema Keter. Mwanachama wa Shirika la Koo za Jamii ya Kipsigis, Joseph Towett Kalyasoi, alisema si jambo la ajabu kwa jamii hiyo kufanya mazishi baada ya jua kutua. “Zamani, miili ilikuwa ikizikwa usiku miongoni mwa jamii ya Kipsigis, ndiyo maana hadi leo baadhi ya shughuli za mwisho za mazishi hufanyika jioni sana. Hii ni mila ya muda mrefu,” alisema. Towett aliongeza kuwa wazazi wa mwanamke aliyeolewa wakiamua kumzika kutokana na tofauti kati yake na mumewe, basi wanapaswa kurejesha mahari iliyolipwa wakati wa ndoa. Wakati huo huo, imebainika kuwa mwili wa Rosemary ulihamishwa kutoka Nairobi kwenda Kericho siku tatu kabla ya mazishi huku mvutano ukiendelea kati ya wazazi wake na mumewe. Chanzo cha familia kilichozungumza kwa siri kilisema hata baadhi ya wanachama wa kamati ya mazishi hawakujua mahali mwili ulikokuwa hadi ulipoondolewa mochari. Ulinzi mkali wa polisi katika makazi ya familia ulivutia hisia za majirani huku ndugu wa karibu wakisimamia taratibu za mazishi. Kwa upande wake, Kimwatu alikuwa ameenda mahakamani kuomba wazazi wa marehemu, Paul Kipkorir Koech na Beatrice Koech, pamoja na dadake Judy Koech-Oyamo na KCB, wazuiwe kuendelea na mipango ya mazishi. Alidai kuwa alikuwa ametengwa katika maandalizi ya mazishi licha ya kuwa mume halali wa Rosemary. Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa wawili hao walifunga ndoa katika Kanisa Katoliki la St Austin mjini Nairobi mnamo Agosti 24, 2013 na walibarikiwa kupata watoto wanne. Kimwatu alikiri kuwa ndoa yao ilikuwa na changamoto lakini akasema walikuwa katika juhudi za kumaliza tofauti zao na waliendelea kuwasiliana mara kwa mara hadi siku ya kifo chake. “Ndoa yetu kwa ujumla ilikuwa ya upendo, furaha na ushirikiano. Kama ndoa nyingine zote, ilikuwa na changamoto zake, lakini hazikuwahi kufikia kiwango cha kuondoa upendo na furaha iliyokuwepo kati yetu,” alisema katika stakabadhi za mahakama. Aliongeza kuwa walikuwa wameachana kwa muda wa miezi minne pekee na kwamba kabla ya kifo chake, Rosemary alikuwa amekubali kurejea nyumbani kwa familia yao. Kimwatu alisema kuwa kama mume wa kisheria alikuwa na haki ya kupanga mazishi ya mkewe na alikusudia kumzika katika makazi ya familia yao huko Matasia, Ngong, Kaunti ya Kajiado. Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena mahakamani Agosti 31 huku maswali yakisalia kuhusu utekelezaji wa amri ya mahakama na uhalali wa mazishi yaliyofanyika Kericho.