Mchujo ODM: Kivumbi 5 kutoka familia ya Odinga wakilenga nyadhifa mbalimbali 2027
ODM inakabiliwa na mtihani mgumu katika uteuzi wa 2027 huku wanachama wa familia ya Odinga wakijitokeza kuwania nyadhifa mbalimbali, hali inayotarajiwa kuzua ushindani mkali ndani ya chama.
Kuingia kwa Raila Junior, mwanawe marehemu kiongozi wa ODM Raila Odinga, katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Kibra kumeibua mjadala kuhusu iwapo familia ya Odinga itaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya hata baada ya kifo cha Raila.
Mbali na Junior, Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga, 82, atatetea kiti chake cha useneta wa Siaya. Katika uteuzi wa chama, atakabiliana na aliyekuwa Gavana wa Siaya Amoth Rasanga.
“Hata kama wewe ni rafiki yangu, hata kama una pesa, usifikiri kwamba pesa zinaweza kununua uongozi. Tutahakikisha kunakuwa na ushindani huru na wa haki,” akasema Dkt Oginga akiwahakikishia wawaniaji wote kuwa uteuzi utakuwa huru
Bw Rasanga, ambaye ni mwanachama wa ODM, ameonya kuwa atatumia njia nyingine kuwania kiti hicho iwapo uteuzi wa chama hautakuwa wa haki na utampendelea Dkt Oginga.
“Mimi ni mwanachama wa ODM maisha yote. Wakipendekeza mimi, sawa. Wasipofanya hivyo, nina njia nyingine,” akasema
Kibra pia inatarajiwa kuwa uwanja wa vita baada ya Junior, 46, kuanza kufanya mikutano na wazee, makundi ya kijamii, madiwani na wanasiasa wanaounga mkono azma yake.
“Kibra ilikuwa ngome ya kisiasa ya babangu, na kama familia tumekuwa na safari ndefu pamoja na watu wa eneo hili. Nikichaguliwa, nitalenga zaidi elimu kwa kuhakikisha kwamba ufadhili wa masomo unapatikana ili kusiwe mtoto anayekosa elimu,” Junior aliambia Taifa Leo.
Alisema pia atajitahidi kuboresha huduma za afya na maji pamoja na maisha ya wakazi wa Kibra.
Mamake, Ida Odinga, alimpa Junior baraka za kuingia katika siasa, lakini akamsihi afanye siasa safi zisizo na matusi, vurugu au fujo.
“Enyi watu wa Kibra mmeamua na sina chaguo jingine. Namkabidhi mwanangu mikononi mwenu. Viongozi mlio hapa, mtunze, mumfundishe na mumwongoze,” akasema Mama Ida.
Junior atakabiliana na Mbunge wa sasa Peter Orero na aliyekuwa mbunge Imran Okoth. Orero amesema anaamini uteuzi utakuwa wa haki na yuko tayari kushindana na Junior.
“Aje tushindane, lakini kwa hali ilivyo sasa, kazi ambayo nimefanya itafanya mambo kuwa magumu kwa wale wanaomsukuma. Hawezi kunishinda kwa sababu kazi ambayo nimefanya inaonekana,” akasema Bw Orero.
Imran, kwa upande wake, ametishia kuondoka ODM na kuwania kama mgombea huru iwapo hakutakuwa na uteuzi wa haki.
“Junior yuko huru kuja kushindana, lakini anapaswa pia kujua kwamba tumekuwa kwa chama na tunasisitiza kwamba kusiwe na mapendeleo,” akasema.
Winnie Odinga anahusishwa na kinyang’anyiro cha useneta Nairobi, ingawa hajathibitisha rasmi azma hiyo.
“Kwa sasa napanga makumbusho ya babangu. Orero ambaye alisema nalenga useneta ananitakia mema,” akaambia Taifa Leo kwenye ujumbe.
Ikiwa atawania, atakabiliana na Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor, ambaye tayari ameanza kampeni.
Kisumu, Ruth Odinga analenga ugavana na anakabiliwa na wapinzani wenye uzoefu, akiwemo Joshua Oron, Aduma Owuor, Naibu Gavana Mathews Owili, Seneta Tom Ojienda na Rosa Buyu.
“Ninachotaka ni ushindani sawa ili aliye bora ashinde,” alisema Ruth.
Jaoko Oburu, mwanawe Dkt Oburu, anaripotiwa kulenga ubunge wa Bondo, ingawa hakupatikana kuthibitisha azma hiyo. Ingawa hivyo, amekuwa akishiriki miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo na kisiasa katika eneobunge hilo.
Akijitosa, atakabiliana na Mbunge Gideon Ochanda, mfanyabiashara Andiwo Mwai na mwanahabari wa Nam Lolwe FM Haron John.
Uwanizi huu wa jamaa umezua kumbukumbu za jinsi Raila alivyokuwa akiingilia kati migogoro ya kisiasa ndani ya familia.
Kabla ya uchaguzi wa 2013, Raila aliingilia mzozo kati ya Dkt Oburu na James Orengo kuhusu useneta wa Siaya, na Dkt Oburu akahamia katika kinyang’anyiro cha ugavana.
Baada ya mzozo katika uteuzi wa ugavana na William Oduol (sasa naibu gavana wa Siaya), Cornel Rasanga alipewa tiketi ya ODM bila kushiriki mchujo, huku Dkt Oburu akipewa nafasi ya kuwania ubunge.
Mnamo 2017, Dkt Oburu alishawishiwa kutowania kiti chochote na badala yake akateuliwa kuwa mbunge wa EALA.
Ruth naye mnamo 2013 alilazimika kuridhika na nafasi ya naibu gavana wa Kisumu baada ya mzozo wa uteuzi wa ODM kati yake na Jack Ranguma.