Matumizi mbegu bora yafika Malagosi, Mgama, Magulilwa

Habari Leo
Published: Sep 02, 2026 17:03:48 EAT   |  News

IRINGA: KILIO cha wakulima cha kupata mbegu bora kwa bei nafuu kimeendelea kupata majibu, huku wakulima katika Wilaya ya Iringa wakisema hatua ya serikali ya kusogeza mbegu bora karibu na mashamba yao imewapa matumaini mapya ya kuongeza uzalishaji na kipato. Wakulima hao wamesema upatikanaji wa mbegu bora, ukienda sambamba na matumizi sahihi ya mbolea na …

IRINGA: KILIO cha wakulima cha kupata mbegu bora kwa bei nafuu kimeendelea kupata majibu, huku wakulima katika Wilaya ya Iringa wakisema hatua ya serikali ya kusogeza mbegu bora karibu na mashamba yao imewapa matumaini mapya ya kuongeza uzalishaji na kipato.

Wakulima hao wamesema upatikanaji wa mbegu bora, ukienda sambamba na matumizi sahihi ya mbolea na kanuni bora za kilimo, unaweza kubadili uzalishaji wa mashamba yao na kuwawezesha kuzalisha chakula cha kutosha kwa familia na ziada kwa ajili ya soko.

Kauli hizo zimetolewa wakati wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mbegu bora inayofanywa na kampuni ya Mgongolwa Agrovet and Seeds ambayo pia ni Wakala wa Mbegu za Serikali (ASA) iliyofanyika katika vijiji vya Malagosi, Mgama na Magulilwa wilayani Iringa.

Katika vijiji hivyo wakulima wamepewa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu zilizoidhinishwa badala ya kutegemea mbegu zisizojulikana ambazo zinaweza kuwa chanzo cha hasara shambani.

Kwa wakulima hao, hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa juhudi za serikali chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan za kumsaidia mkulima kuongeza tija, badala ya kuendelea kulima kwa kutegemea mbegu zisizo na uhakika wa mavuno.

Mkulima wa kijiji cha Malagosi, Lucy Mwenda, amesema amefurahishwa na hatua ya Serikali kusogeza mbegu bora kwa wakulima, akisema upatikanaji wake kwa bei nafuu utawasaidia kuanza msimu wa kilimo wakiwa na matumaini makubwa.

“Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha wakulima wa Malagosi. Mbegu hizi zitatatusaidia kuongeza mavuno na kutuwezesha kukidhi mahitaji yetu,” amesema Mwenda.

Hata hivyo, Mwenda amesema changamoto nyingine kubwa inayowakabili wakulima ni gharama za mbolea, akiiomba Serikali kuendelea kuangalia namna ya kupunguza mzigo huo ili mkulima aweze kumudu gharama za uzalishaji.

Amesema kwa mkulima, mbegu bora pekee haitoshi ikiwa gharama za pembejeo nyingine zitaendelea kuwa kubwa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika vijiji hivyo, Mkurugenzi wa Mgongolwa Agrovet and Seeds, Joseph Mgongolwa amesema matumizi ya mbegu bora ni moja ya hatua muhimu katika kuongeza tija ya kilimo.

Taarifa za ASA zinaonyesha kuwa Wakala huo una jukumu la kuhakikisha upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora kwa wakulima, pamoja na kushirikiana na sekta binafsi katika kuongeza uzalishaji na usambazaji wa mbegu nchini.

Mgongolwa amesema wakulima wanapaswa kuchagua mbegu kwa kuzingatia aina ya zao, mazingira ya eneo husika na ushauri wa wataalamu wa kilimo, badala ya kuangalia bei pekee.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika kampeni hiyo, wakulima wameelekezwa kuhusu mbegu mbalimbali zikiwemo za mahindi ya muda mfupi na hybrid, alizeti, mpunga, maharage ya njano na mekundu pamoja na ufuta.

Amesema matumizi ya mbegu bora yanapaswa kuambatana na maandalizi mazuri ya shamba, upandaji kwa wakati, matumizi sahihi ya mbolea na ufuatiliaji wa shamba ili mkulima aweze kupata matokeo yanayotarajiwa.

Mgongolwa pia amewataka wakulima kuwa makini na watu wanaouza mbegu zisizo na uhakika, akisema mbegu feki zinaweza kumrudisha nyuma mkulima baada ya kutumia muda, nguvu na fedha kulima.

Amesema wakulima wanapaswa kununua mbegu kutoka kwa wauzaji wanaotambulika na kuhakikisha vifungashio vina taarifa muhimu zinazoweza kusaidia kuthibitisha ubora na uhalali wa mbegu.

Mkulima Wema Mbalinga amesema upatikanaji wa mbegu kwa bei nafuu umewapa wakulima matumaini ya kuongeza mavuno na kuboresha maisha yao.

“Rais Samia tunamshukuru kwa kusikia kilio cha wanyonge na kutuletea mbegu yenye ruzuku. Tulikuwa wanyonge sana. Tunaamini mbegu hizi zitatusaidia kuongeza uzalishaji,” amesema Mbalinga.

Hata hivyo, amesema pamoja na mbegu, wakulima bado wanahitaji ulinzi katika soko la mazao yao, akiiomba Serikali kuendelea kusimamia suala la lumbesa ambalo amesema limekuwa likiwaongezea hasara wakulima wakati wa kuuza mazao.

Kwa mujibu wa Mbalinga, mkulima mwenye uhitaji wa fedha wakati wa mavuno huwa katika mazingira magumu ya kujadiliana na mnunuzi, hivyo usimamizi madhubuti wa biashara ya mazao ni muhimu ili mkulima apate thamani inayostahili ya jasho lake.

Mkulima Ernest Busyanati amesema bei ya mbegu inayopatikana kupitia mpango huo itawapa wakulima nafasi ya kuanza msimu bila mzigo mkubwa wa gharama.