Matogoro; Hifadhi ya msitu asilia  iliyobeba fahari ya utalii

Habari Leo
Published: Jul 28, 2025 09:57:34 EAT   |  Travel

RUVUMA; HIFADHI ya Msitu wa Matogoro iko Kusini Mashariki mwa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, takribani kilometa 15 kutoka Songea mjini. Msitu huu umezungukwa na vijiji vya Ndilima na Litembo kwa upande wa Magharibi na Mahilo na Mpingi kwa upande wa Mashariki. Upande wa Kusini kuna Kijiji cha Lipaya na Matogoro kwa upande wa Kaskazini. …

RUVUMA; HIFADHI ya Msitu wa Matogoro iko Kusini Mashariki mwa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, takribani kilometa 15 kutoka Songea mjini.

Msitu huu umezungukwa na vijiji vya Ndilima na Litembo kwa upande wa Magharibi na Mahilo na Mpingi kwa upande wa Mashariki.

Upande wa Kusini kuna Kijiji cha Lipaya na Matogoro kwa upande wa Kaskazini. Msitu huo una ukubwa hekta 7,457.

Machi 22, 2023 serikali iliupandisha hadhi Msitu wa Matogoro kuwa Msitu wa Hifadhi wa Asili na kuufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa na misitu miwili ya hifadhi ya asili baada ya ule wa Mwambesi ulioko Wilaya ya Tunduru, yote ikiwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Msitu huo unaelezwa kuwa ni kivutio adhimu cha utalii lakini pia chanzo cha maji cha mito miwili maarufu nchini ambayo ni Mto Ruvuma wenye urefu wa zaidi ya kilometa 800 ambao unaomwaga maji yake Bahari ya Hindi na unaunganisha nchi za Tanzania na Msumbiji.

Aidha, msitu huo pia ni chanzo cha Mto Luhira ambao pia ni chanzo cha Mto Ruhuhu unaomwaga maji yake katika Ziwa Nyasa. Mto Ruhuhu unachangia asilimia 20 ya maji katika Ziwa Nyasa.

Ofisa Utalii katika Hifadhi ya Msitu Asilia Matogoro, Arafa Saidi anasema katika hifadhi hiyo kuna vivutio vingi ikiwemo chanzo cha Mto Ruvuma na uoto wa asili unaotengeneza mandhari nzuri ya kuvutia na yenye kutuliza akili kwa mtu anayetembelea msitu huo.

“Kwenye uoto wa asili tunasemea miti, maua aina mbalimbali za kuvutia na hali ya hewa kwa ujumla. Kivutio kingine tulicho nacho katika hifadhi yetu tumebahatika kuwa na mapango ambayo yalitumika kujificha watu katika kipindi cha Vita ya Majimaji,” anasema Arafa.

Anasema kwa sasa mapango hayo yanatumiwa na wenyeji wa maeneo mbalimbali ya mkoa huo kufanya matambiko na shughuli mbalimbali za jadi zikiwemo za tiba.

Arafa anasema shughuli mbalimbali za utalii zinafanyika ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Matogoro ikiwemo utalii wa kutembea msituni, utalii wa kupanda mlima na kuona ndege kwa kuwa msitu huo umejaaliwa utajiri wa ndege wa aina mbalimbali wengine wakiwa ni wale wanaohamia kutoka Ulaya na kurejea.

“Tunao wanyamapori wadogo wa aina mbalimbali na hali ya hewa ya kipekee kwa sababu hali ya hewa iliyopo kwenye hifadhi yetu ni tofauti na inayopatikana mjini (Songea).”

Kwa upande wa uoto wa asili, hifadhi yetu imezungukwa na miti mingi aina ya miombo, misuku na mibuna.

Arafa anasema mtalii anapofika katika hifadhi hiyo, ana uwezo wa kuweka kambi na kukaa kwa siku kadhaa akifanya shughuli za utalii kwani lipo eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya kuweka mahema ya kambi ya utalii lenye huduma zote muhimu.

“Uwezekekano wa kuweka kambi tumeweka katika makundi mawili. Kama mtalii ana vifaa vyake tunampatia eneo ambalo lina vitu vyote muhimu ambavyo vinahitajika katika utalii wa kambi ikiwa ni pamoja na umeme, maji huduma za mawasiliano na usalama,” anasema Arafa.

Anaongeza: “Kama hana vifaa sisi tunamsaidia vifaa kuanzia mahema, magodoro na kama atahitaji huduma za chakula pia tunampatia kulingana na makubaliano tutakayowekeana naye na vyakula atakavyotaka.”

“Kitu ambacho watu wengi hawajakifahamu kuhusu Matogoro ni kwamba, hii ni hifadhi ya asili inayopatikana ndani ya Manispaa ya Songea, yani iko mjini si mbali na mji, kitu ambacho kinaitofautisha na hifadhi nyingine,” anaeleza.

Anasema mtu ambaye ana lengo la kupata utulivu wa kutafakari, kupata mawazo mapya na kupata hewa nzuri ndani ya hifadhi, hiyo ndiyo eneo sahihi kwa sababu ni sehemu tulivu yenye vitu vya asili.

“Sauti unazosikia huku ni sauti za asili huwezi kusikia sauti ya gari kwa sababu hakuna magari yanayopita labda liwe limeleta mgeni, huku sauti ni zile ya wanyama, ndege au upepo,” anabainisha.

Fursa

Kuhusu fursa zinazopatikana katika hifadhi hiyo, Arafa anasema ziko fursa nyingi katika hifadhi hiyo ambazo watu wanaweza kujitokeza na kuwekeza.

“…Unaweza kuwekeza kwenye michezo ya watoto, unaweza kuwekeza kwenye eneo la kufanyia matukio mbalimbali kama sherehe, kwa hiyo unaweza kuwekeza kwa kujenga kama ukumbi wa sherehe na vikao,” anasema.

“Pia kama kuna mtu anaweza kuwekeza kwenye malazi yaani zile nyumba za kulala wageni ambazo ni rafiki kwa mazingira, nyumba ambazo zitakuwa ndani ya hifadhi yetu ambazo tuna uhakika haziwezi kuharibu mazingira,” anaongeza Arafa.

Anafafanua kuwa, kwa uwepo wa nyumba hizo za kulala wageni, hudumza za chakula zitahitajika kwa kiwango kikubwa.

“Pia kama kutakuwa na nyumba za kulala wageni, eneo lingine la uwekezaji litakuwa ni kwenye restauranti ambayo itakuwa inatoa huduma za vyakula na vinywaji,” anasema.

Gharama za kuingia na kufanya utalii katika hifadhi hiyo kwa watalii wa ndani ni pamoja na kiingilio cha Sh 3,000 kwa wakubwa na 1,500 kwa watoto wa kuanzia miaka mitano, chini ya miaka mitano ni bure.

Kwa upande wa watalii wa kutoka nje ya nchi, kiingilio ni Sh 30,000 kwa wakubwa na 15,000 kwa watoto wa kuanzia miaka mitano na wa chini ya miaka mitano ni bure.

Katika moja ya hotuba alizowahi kutoa, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula anasema Hifadhi ya Msitu Asili Matogoro yenye mandhari ya kuvutia ni kichocheo adhimu na muhimu cha kukuza utalii katika mikoa ya Kusini hususani Ruvuma kutokana na kubeba hazina kubwa ya kihistoria ikiwemo ya uwepo wa mapango makubwa yaliyotumika wakati wa Vita ya Majimaji.

Anasema hifadhi hiyo imebeba jukumu kubwa la uhai na ustawi wa Watanzania kutokana na ukweli kuwa, ni chanzo cha mito mitatu mikubwa na muhimu ambayo ni Ruvuma unaomwaga maji yake katika Bahari ya Hindi, Luwegu ambao unachangia asilimia 19 ya maji kwenye Mto Rufiji na kisha kuingia Bahari ya Hindi.

Mto Luhira ambao ni chanzo cha Mto Ruhuhu unamwaga maji yake kwenye Ziwa Nyasa.

Anatoa mwito kwa wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika eneo hilo lenye mandhari nzuri na ya kuvutia inayofaa kwa utalii wa kupanda milima, utalii wa picha, utalii wa kuruka kwa na utalii wa ikolojia.