Mapambano dawa za kulevya yaendelea kuzaa matunda
DODOMA: Serikali imesema imeendelea kupata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kutokana na kuimarika kwa operesheni za udhibiti, ushirikiano wa vyombo vya dola pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii. Hayo yameelezwa leo Mei 29, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye …
The post Mapambano dawa za kulevya yaendelea kuzaa matunda first appeared on HabariLeo.
DODOMA: Serikali imesema imeendelea kupata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kutokana na kuimarika kwa operesheni za udhibiti, ushirikiano wa vyombo vya dola pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii.
Hayo yameelezwa leo Mei 29, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2025 aliyoiwasilisha bungeni.
Profesa Kabudi amesema uwasilishaji wa taarifa hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 66 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 kinachoitaka Serikali kuwasilisha taarifa hiyo kila mwaka bungeni.
Amesema taarifa hiyo inalenga kuonesha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi kupitia Bunge pamoja na kutoa tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti dawa za kulevya nchini.
“Mwaka 2025 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan iliendelea kuwekeza nguvu kubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema mwaka 2025 bangi iliendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi ambapo tani 1,017.26 zilikamatwa, ingawa kiwango hicho kilipungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, kupungua huko kumechangiwa na uteketezaji wa mashamba makubwa ya bangi uliofanyika mwaka 2024 pamoja na kuongezeka kwa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya kilimo hicho.
Aidha amesema tani 26.36 za mirungi zilikamatwa mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka uliopita kutokana na kuimarika kwa operesheni za udhibiti hususan mipakani.
Katika dawa za kulevya za viwandani, Serikali ilikamata kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin, kilogramu 4.89 za cocaine, gramu 178 za MDMA pamoja na gramu 7.82 za MDA.
Profesa Kabudi amesema kwa mara ya kwanza mwaka 2025 Serikali ilifanikiwa kukamata tani 29.52 za dawa mpya aina ya Kratom inayotokana na mmea wa Mitrogyna speciosa baada ya kuingizwa nchini ikidaiwa kuwa mbolea.
“Mafanikio haya yametokana na kazi kubwa inayofanywa na mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti mitandao ya usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia nchi kavu, anga na majini,” amesema.
Amesema Serikali pia iliendelea kuimarisha ukaguzi katika vituo vya forodha, vyombo vya usafiri, kampuni za usafirishaji vifurushi pamoja na kampuni zinazojihusisha na biashara ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Kupitia ukaguzi huo, tani 31.76 na lita 183.5 za kemikali bashirifu pamoja na kilogramu 2.36 na mililita 160 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa.
Kuhusu mashauri ya dawa za kulevya, Profesa Kabudi amesema mwaka 2025 jumla ya mashauri 1,124 yalifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini huku mashauri 1,373 yakitolewa hukumu ambapo Jamhuri ilishinda mashauri 1,058.
Aidha mali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.3 zilizohusishwa na makosa ya dawa za kulevya zilitaifishwa.
Katika huduma za tiba na utengamao, amesema watu 85,425 wenye uraibu wa dawa za kulevya walipata huduma katika vitengo vya afya ya akili, kliniki za MAT pamoja na nyumba za upataji nafuu nchini.
Pia Serikali iliendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya kupitia kampeni mbalimbali katika jamii, taasisi za elimu na vyombo vya habari.
Profesa Kabudi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kujenga uwezo wa kitaasisi na kuendesha operesheni za pamoja dhidi ya mitandao ya biashara ya dawa za kulevya.
Amewapongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama, wataalamu wa afya pamoja na wananchi kwa ushirikiano wao katika mapambano hayo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo husika pale wanapobaini viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya ili kuifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya tatizo hilo.
The post Mapambano dawa za kulevya yaendelea kuzaa matunda first appeared on HabariLeo.