Maofisa ugani Mtwara kupewa elimu ya viuatilifu

Habari Leo
Published: Jun 06, 2025 09:51:22 EAT   |  Educational

MTWARA: MAOFISA ugani 569 mkoani Mtwara wanatarajia kupatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya zao la korosho katika msimu wa kilimo mwaka 2025/2026. Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele, Bakari Kidunda amesema uzalishaji wa korosho umekuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ambapo moja …

MTWARA: MAOFISA ugani 569 mkoani Mtwara wanatarajia kupatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya zao la korosho katika msimu wa kilimo mwaka 2025/2026.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele, Bakari Kidunda amesema uzalishaji wa korosho umekuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ambapo moja ya changamoto kubwa ikiwemo utambuzi na udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu wa zao hilo.

Lengo la mafunzo ni kwamba wanapoelekea msimu wa upuliziaji wa mikorosho katika msimu huo ni kuwakumbusha juu ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu kwenye zao la korosho ili kuleta tija katika uzalishaji, yaliyofanyika eneo la Mbawala chini Kata ya Naliendele Manispaa ya Mtwara Mikindani.

‘’Hii ni miongoni mwa changamoto kubwa, tukifanya vizuri katia eneo hili tutapelekea kuongezeka uzalishaji wa zao la korosho, tukifanya vibaya kwenye eneo hili moja kwa moja tutapelekea kushuka kwa uzalishaji,’’amesisitiza Kidunda.

Maafisa ugani washauriwa kutoa utalaamu kilimo

Aidha, lengo la serikali ni kuzalisha tani laki 7 katika msimu huo wa mwaka 2025/2026 na tani milioni 1 mwaka 2030 hivyo ili wafikie malengo hayo ni lazima waweke mikakati ya kuweza kupambana ili waweze kuongeza uzalishaji huo mbapo moja ikiwemo suala la utoaji wa elimu hiyo.

Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Geofrey Mwalembe amesema katika msimu huo wa mwaka 2025/2026 wanaendelea na utoaji wa mafunzo hayo kwa maofisa ugani hao ambapo kwa awamu ya kwanza yanafanyika katika mkoa huo wa Mtwara pamoja na mkoa wa Lindi.

Amesema kwa mkoa wa Mtwara, katika maofisa ugani hao 569 wanaopatiwa mafunzo kati yao 245 ni wale waliyoajiriwa na Cbt chini ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) wengine 323 waliyopo ngazi ya halamshauri ambapo lengo ni kuwajengea uelewa kuhusu visumbufu vya zao hilo ili waweze kufikisha elimu hiyo kwa wakulima katika maeneo yao.

Mshauri wa Kilimo Mkoa wa Mtwara, Ally Linjenje amesema serikali imetoa viuatilifu katika mkoa huo ambavyo vinatakiwa vitumike vizuri ili viweze kuleta tija ambapo kwa mwaka huu 2025 mkoa huo umepokea pembejeo za unga tani 21 elfu na viuatilifu vya maji lita laki 8.

Mafunzo hayo yameanza Juni 5, 2025 hadi Juni 16 mwaka huu, yaliyoandaliwa na Tari Naliendele kwa kushirikiana na Cbt pamoja na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara.