Makonda azindua shule mpya Bugumangala

Habari Leo
Published: Oct 12, 2026 13:42:29 EAT   |  News

MWANZA: Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, Oktoba 12, 2026, amezindua Shule Mpya ya Awali na Msingi Bugumangala, iliyopo Kijiji cha Bugumangala, Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza. Ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh milioni 430.7 zilizotolewa na Serikali kupitia Programu ya BOOST katika mwaka wa fedha 2025/2026. Mradi …

MWANZA: Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, Oktoba 12, 2026, amezindua Shule Mpya ya Awali na Msingi Bugumangala, iliyopo Kijiji cha Bugumangala, Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.

Ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh milioni 430.7 zilizotolewa na Serikali kupitia Programu ya BOOST katika mwaka wa fedha 2025/2026. Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutumika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo, Makonda amewapongeza wananchi wa Bugumangala kwa kujitolea zaidi ya hekta saba za ardhi na kutoa nguvu kazi, ikiwemo kusomba mawe, kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Amesema ushirikiano huo umeonesha dhamira ya wananchi katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha upatikanaji wa elimu. Aidha, ameahidi kuchangia bati ili kuendeleza ujenzi na kukamilisha miundombinu iliyobaki kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza mradi huo, akieleza kuwa utapunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zilizopo na kuongeza fursa za elimu ya awali na msingi kwa watoto wa Bugumangala na maeneo jirani.

Amesema shule hiyo itasaidia kuboresha ufaulu, kuongeza ufanisi wa ufundishaji na kuimarisha ustawi wa walimu, huku ikichangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia elimu bora.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani, amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa jengo la utawala, vyumba sita vya madarasa ya msingi, jengo la elimu ya awali lenye vyumba viwili, vyoo na uzio.

Miundombinu mingine ni matundu 10 ya vyoo vya elimu ya msingi pamoja na nyumba moja ya walimu yenye uwezo wa kuhudumia familia mbili.

Ramadhani amesema ujenzi huo pia umewezesha ajira za muda kwa wananchi 87, wakiwemo wanaume 82 na wanawake watano, na kuongeza fursa za kipato kwa walioshiriki katika shughuli za ujenzi.

Amesema kukamilika kwa shule hiyo kutaboresha upatikanaji wa madarasa, huduma za usafi wa mazingira, ofisi za utawala na makazi ya walimu, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa elimu kwa watoto wa eneo hilo.