Mafua yasiyoisha huenda yanaashiria tatizo la kiafya – mtaalam

Taifa Leo
Published: Oct 11, 2026 15:17:16 EAT   |  News

UJAUZITO NA UZAZI

IWAPO mtoto wako anaugua homa isiyoisha hata baada ya kutibiwa, anatatizika kula na kunywa au kushindwa kupumua vizuri, unashauriwa kumpeleka hospitalini atibiwe.

Dalili hizi huenda zinaashiria ugonjwa sugu zaidi ambao haufai kupuuzwa, kulingana na Daktari wa watoto Anne Sheehan.

Misimu ya vuli na kipupwe huashiria kilele cha kipindi cha maambukizi ya mfumo wa kupitishia hewa kama vile homa ya kawaida (common cold), influenza, RSV na Covid-19.

Maradhi haya, anafafanua Dkt Sheehan, aghalabu huanza na dalili zinazofanana sana hivyo ni muhali kuzitofautisha, hasa wakati msimu wa baridi na homa unapoanzia mwishoni mwa kiangazi hivyo kusababisha mizio ya kimsimu.

Mtoto anapougua dalili kama vile kukohoa, kutokwa na kamasi na maumivu ya koo, mtanziko unaomkumbuka kila mzazi ni ama kumruhusu aende shule, akae nyumbani ili apate nafuu au ampeleke hospitalini.

Dkt Sheehan anafafanua kuwa kumruhusu mtoto kwenda shule akiwa anaugua kunaweza kumfanya akae muda mrefu bila kupata nafuu na kusambaza maambukizi yake kwa wanafunzi wenzake na wahudumu wa shule.

“Maambukizi yote haya yanayozuka mara kwa mata yanaweza kusababisha athari sugu kwa baadhi ya wanajamii wa shule – au familia zao – walio na matatizo sugu ya kiafya yanayoweza kuzorotesha hali zao zaidi,” anafafanua Dkt Sheehan katika jarida la The Conversation.

Maambukizi mengi ya mfumo wa kupitishia hewa kwa watoto, kwa kawaida yanaweza kudhibitiwa nyumbani, ikiwemo Covid-19, bila haja ya kwenda hospitalini kila wakati mtoto anapokohoa au kutiririkwa na kamasi, anaeleza.

Hata hivyo, baadhi ya dalili huenda zikaashiria ugonjwa sugu hivyo hupaswi kuzipuuza katu.

Kama mzazi anayemwelewa vyema mtoto wake, ni muhimu kutofautisha iwapo maambukizi ya mafua anayougua mtoto wako ni mafua ya kawaida, flu, RSV au Covid-19, flu, ikizingatiwa kuwa baadhi ya maradhi haya yanaweza kusababisha matatizo sugu kwa baadhi ya watoto.

Covid-19 ina tishio la juu zaidi la kusababisha athari sugu na za muda mrefu kiafya, huku aina nyinginezo za mafua zikiwa na athari finyu, anasema mtaalam huyo wa watoto.

“Mafua aina ya flu yanaweza kusababisha makali ya ugonjwa na kulazwa hospitalini huku RSV ikiwa na uwezekano wa kuwa hatari zaidi hasa kwa malaika, watoto wachanga na wanaougua matatizo sugu kiafya.”